
CHINA: Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Elieneza Nsangazelu, amesema ameridhishwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wake katika ushindi dhidi ya China, akieleza kuwa timu ilitekeleza vyema mpango wa mchezo licha ya ushindani mkubwa.
Katika mechi hiyo Jana, Serengeti iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Nsangazelu amesema Serengeti Boys ilitawala umiliki wa mpira kwa vipindi vingi na kufanikiwa kuwazuia wapinzani kucheza kwa uhuru.
“Tulicheza vizuri na wachezaji walitekeleza majukumu yao kwa nidhamu. Tulifanikiwa kuwabana wapinzani na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga,” amesema.
Amebainisha kuwa timu yake ilitengeneza zaidi ya nafasi 10 za kufunga, ikiwemo mkwaju wa penalti, lakini haikuweza kuzitumia zote.
“Tulipata nafasi nyingi za kufunga, zaidi ya 10, lakini hatukuzitumia ipasavyo. Hata hivyo tunamshukuru Mungu kwa ushindi na tunaona timu inaendelea kupiga hatua,” amesema.
Nsangazelu amesema kila mpinzani ana mfumo na mbinu zake, hivyo benchi la ufundi linaendelea kufanya marekebisho kulingana na aina ya mchezo unaowakabili.
“Kila mpinzani ni tofauti na kila mchezo unahitaji maandalizi tofauti. Tunaendelea kujifunza na kufanya maboresho ili tuwe tayari kwa changamoto zinazofuata,” amesema.
Akizungumzia mchezo ujao dhidi ya Australia, amesema wachezaji watapumzika kwanza kwa ajili ya kurejesha nguvu kabla ya kuanza maandalizi rasmi.
Aliwataka Watanzania kuendelea kuwaunga mkono Serengeti Boys, akisema sapoti yao ndiyo inayowapa hamasa ya kupambana na kupeperusha bendera ya taifa.




