Kwingineko

Mashabiki Chelsea wawaka hasira, wamgeukia mmiliki

LONDON: HALI ya sintofahamu imezidi kutanda ndani ya klabu ya Chelsea kufuatia kuongezeka kwa hasira za mashabiki dhidi ya umiliki wa BlueCo, huku kauli mbiu ya “Hatujali Clear lake, nao hawatujali sisi” ikiendelea kutawala majukwaa ya Stamford Bridge msimu huu.

Hasira hizo zimechochewa zaidi na kipigo cha mabao 3-1 walichopata dhidi ya Nottingham Forest katika mchezo wa Ligi Kuu England, matokeo ambayo yamefuta kabisa matumaini ya kumaliza katika nafasi ya tano na kuifanya timu hiyo kuwa mbali na lengo lao la awali la kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kwa sasa, Chelsea inaonekana kupoteza mwelekeo huku mashabiki wakizidi kuonesha kutoridhishwa na uongozi wa BlueCo, kampuni inayomilikiwa na Todd Boehly pamoja na wawekezaji wake, ikiwemo Clearlake Capital.

Mbali na matokeo mabaya uwanjani, pengo kati ya mashabiki na uongozi limekuwa kubwa zaidi kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha—Chelsea ikiwa katika harakati za kutafuta kocha wake wa sita wa kudumu ndani ya kipindi cha miaka minne, baada ya kumfuta kazi Liam Rosenior mwezi uliopita.

Pia, kumekuwa na malalamiko kuhusu kiwango cha kujituma kwa baadhi ya wachezaji pamoja na sera za tiketi, hali inayozidi kuwakasirisha wafuasi wa klabu hiyo.

Kifedha, hali si nzuri pia baada ya ripoti za hivi karibuni kuonesha hasara ya pauni milioni 262 kabla ya kodi rekodi mbaya zaidi katika Ligi Kuu England huku UEFA ikiendelea kufuatilia matumizi ya klabu hiyo chini ya makubaliano maalum ya udhibiti wa matumizi ya fedha.

Kutokana na hali hiyo, kundi la mashabiki linalojiita “Not A Project CFC” limeibuka na kuwa sauti ya upinzani, likihamasisha mabadiliko makubwa ndani ya klabu. Tayari wamepanga maandamano mawili, likiwemo moja litakalofanyika kabla ya fainali ya FA Cup dhidi ya Manchester City, pamoja na lingine ambapo mashabiki wanahimizwa kugeuza migongo yao dakika ya 22 katika mechi dhidi ya Tottenham Hotspur ikiashiria mwaka 2022 ambao BlueCo ilinunua klabu hiyo kutoka kwa Roman Abramovich.

Licha ya baadhi ya viongozi wa ndani ya klabu kujaribu kutuliza hali hiyo, ikiwemo mkurugenzi Danny Finkelstein aliyewahi kueleza kuwa Chelsea inajenga moja ya timu bora duniani, bado mashabiki wengi hawaoni matumaini ya haraka.

Kwa sasa, Chelsea ipo nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi ikiwa imesalia na michezo mitatu, huku macho yakielekezwa kwenye fainali ya FA Cup kama tumaini pekee la kuokoa msimu.

Related Articles

Back to top button