Kwingineko

Netflix Kutumia Dola Bilioni 1 Kuzalisha Filamu Mexico

MEXICO:Mtandao wa Netflix umetangaza mpango wa kutumia dola bilioni 1 kwa muda wa miaka minne kutengeneza filamu na mfululizo wa tamthilia nchini Mexico. Hatua hii inalenga kuimarisha juhudi za serikali ya Mexico kuvutia uwekezaji na kukabiliana na vitisho vya ushuru kutoka Marekani.

Mtendaji Mkuu Mwenza wa jukwaa hilo la utiririshaji maudhui, Ted Sarandos, alitoa tangazo hilo katika mkutano na waandishi wa habari akiwa na Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum. Sheinbaum alisifu mpango huo, akiuita ushindi kwa uchumi wa pili kwa ukubwa katika Amerika Kusini.

Sarandos alisema kuwa Mexico ni nyumbani kwa makao makuu ya Netflix kwa Amerika ya Kusini:
“Rais Sheinbaum, tunatarajia kufanya kazi na wewe na timu yako ili siyo tu kukuza uchumi na kutengeneza fursa, bali pia kuendeleza utamaduni na urithi huu mzuri wa Mexico ulimwenguni.”

Sarandos alieleza mafanikio ya matoleo ya awali ya Netflix nchini Mexico, akimtolea mfano Alfonso Cuarón, ambaye alishinda tuzo ya Oscar mwaka 2018:
“Kwa miaka mingi, tumefanya kazi na mamia ya waundaji wa maudhui wa Mexico kwenye mamia ya hadithi na filamu zilizovutia hadhira kubwa nchini. Hii ina maana kwamba tunawekeza katika jumuiya ya wabunifu, kusaidia watu wenye vipaji kupata nafasi katika sekta yetu, lakini pia tunachangia sekta nyingine kama upishi, hoteli, usafiri na viwanda.”

Alisema kuwa utengenezaji wa hivi karibuni wa filamu Pedro Páramo umechangia dola milioni 18 kwa uchumi wa Mexico na kutoa ajira kwa maelfu ya watu. Tangazo hilo linakuja siku chache baada ya Rais Sheinbaum kukaribisha uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 2 kutoka benki kubwa ya Uhispania, Santander, kwa kipindi cha miaka mitatu.

Mwezi uliopita, Sheinbaum aliwasilisha mpango wa kuigeuza Mexico kuwa miongoni mwa nchi 10 zenye uchumi mkubwa duniani, akilenga kuvutia uwekezaji wa dola bilioni 277.

Serikali yake pia inajaribu kuepuka ushuru wa asilimia 25 unaotishiwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, kwa kuongeza ushirikiano katika vita dhidi ya mtiririko haramu wa dawa za kulevya na wahamiaji.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button