Ligi Kuu

Nsajigwa ana matumaini Prisons kubaki Ligi Kuu

MBEYA: KOCHA Mkuu wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa, amesema bado ana matumaini timu yake kubaki katika Ligi Kuu licha ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Mbeya City katika mchezo wa mtoano wa kuwania nafasi ya kubaki ligi hiyo.

Matokeo hayo yameihakikishia Mbeya City kuendelea kushiriki Ligi Kuu msimu ujao. Ni baada ya awali kushinda mabao 2-0, huku Tanzania Prisons ikilazimika kucheza mchezo mwingine wa mtoano dhidi ya Polisi Tanzania ya Championship kuwania tiketi ya mwisho ya kubaki kwenye ligi hiyo.

Akizungumza baada ya mchezo, Nsajigwa amesema timu yake ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini ilishindwa kuzitumia.

“Tulijitahidi kutengeneza nafasi nyingi, lakini hatukuwa makini katika umaliziaji. Kama tungezitumia nafasi za mapema, matokeo yangekuwa tofauti. Mbeya City walipata nafasi chache na wakazitumia vizuri zaidi,” amesema.

Amesisitiza kuwa bado hawajakata tamaa na sasa wataelekeza nguvu zao katika mchezo ujao dhidi ya Polisi Tanzania.

“Bado tuna nafasi. Tumebakiwa na mchezo mmoja muhimu wa kupigania nafasi ya kubaki Ligi Kuu. Kikubwa ni kujipanga vizuri na kuhakikisha tunatumia nafasi tutakazopata,” anesema.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button