Filamu

Balozi Yakubu, TFB na Ufaransa waweka mikakati kukuza sekta ya filamu

DAR ES SALAAM: BALOZI wa Tanzania nchini Ufaransa, Saidi Othman Yakubu, na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania (TFB), Dk. Gervas Kasiga, wameweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ufaransa kwa lengo la kukuza sekta ya filamu na kuitangaza Tanzania kimataifa.

Katika kikao kilichofanyika katika Ubalozi wa Tanzania mjini Paris, viongozi hao walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano kupitia kubadilishana uzoefu, kuvutia uwekezaji katika tasnia ya filamu, pamoja na kuanzisha ushirikiano rasmi kati ya TFB na taasisi mbalimbali za filamu nchini Ufaransa.

Pia walikubaliana kuhamasisha ushiriki wa Bodi ya Filamu Tanzania na wadau wake katika matamasha na maonesho ya filamu yanayofanyika nchini Ufaransa na Tanzania, hatua inayolenga kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utengenezaji wa filamu na maudhui ya ubunifu barani Afrika.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Yakubu alisema Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa utaendelea kuwa daraja la kuwaunganisha wadau wa sekta ya ubunifu kutoka mataifa hayo mawili ili kuimarisha ushirikiano, kuvutia uwekezaji na kufungua masoko mapya kwa watayarishaji wa filamu wa Tanzania.

Kwa upande wake, Dkt. Kasiga alisema TFB imejipanga kupanua ushirikiano wa kimataifa ili kuongeza ubora na ushindani wa tasnia ya filamu nchini, huku sekta hiyo ikitoa mchango mkubwa zaidi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Ameeleza kuwa ushirikiano huo unatarajiwa kufungua fursa za mafunzo, ubadilishanaji wa teknolojia, uzalishaji wa pamoja wa filamu na kuongeza ushiriki wa wadau wa filamu wa Tanzania katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button