Robertson:Hatuna kisasi na Real Madrid
LIVERPOOL: BEKI wa Liverpool Andy Robertson amesisitiza kwamba hatauendea mchezo wa leo usiku wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi Real Madrid akiwa na nia ya ‘kulipiza kisasi’ akilini.
Beki huyo wa kushoto wa Scotland alikuwa sehemu ya Liverpool mara zote ambazo Liverpool ilipoteza kwa wababe hao wa La Liga katika fainali za Ligi ya Mabingwa 2018 na 2022. Robertson pia aliondoshwa na Madrid katika robo fainali ya 2021 na mwaka 2023 raundi ya 16 bora.
Robertson aliviambia vyombo vya habari kuwa haangalii kabisa uwezekano wa kulipiza kisasi kwa Real Madrid au kufanya kitu kunachofanana na hicho na kusema kuwa michezo ya hapo awali baina yao ilikuwa tofauti.
“Nadhani mwaka 2018 ulikuwa muhimu sana kwa safari yetu. Hakuna aliyetarajia tungeshiriki fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka huo, na ilitupa imani kwamba tunaweza kushindana tena na kuendelea na kushinda mwaka ujao, ambayo ilikuwa muhimu sana.”
“Mwaka 2022 ni dhahiri ulituumiza zaidi wakati huo nilifikiri tulicheza vizuri, nilidhani tulitawala mchezo. Kipa wao alikuwa mchezaji bora wa mechi, ambayo inakuambia mengi. Lakini mara nyingi wanafanya kile wanachofanya, kuna sababu kwa nini wametwaa kombe hilo zaidi ya timu yoyote ile”amesema Robertson.