Collina: Hakuna anayeweza kuhoji uadilifu wa waamuzi Kombe la Dunia

GEORGIA: Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya FIFA, Pierluigi Collina, ametoka hadharani na kufafanua sababu za kukataliwa kwa bao la Misri dhidi ya Argentina baada ya mapitio ya VAR kwenye mchezo wa Kombe la Dunia 2026.
Collina ameeleza hayo baada ya Shirikisho la Soka Misri (EFA), kumlaumu mwamuzi wa mechi hiyo ya hatua ya 16 Bora, Francois Letexier kuwa ni chanzo cha wao kupoteza mabao 3-2.
Pia, Kocha wa Misri, Hossam Hassan alieleza kuona upendeleo kwa Argentina katika mechi hiyo, akisema: “Pengine wanataka kuendelea kumuweka bingwa wa dunia kwenye michuano.”
Aidha, kupitia taarifa iliyowekwa na Mtandao wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Collina ameeleza kuwa baada ya kila bao, mfumo wa VAR hukagua mchakato mzima wa shambulizi, na hakuna kikomo cha umbali kutoka lilipo goli au muda uliopita tangu tukio litokee.
Katika marudio hayo, ilibainika wazi kuwa mchezaji wa Misri, Marwan Attia, alimkanyaga mguu beki Lisandro Martinez, na kwa mujibu wa sheria, kosa ni kosa tu hata kama lilitokea kabla ya goli.
Aidha, Colina alisisitiza: “Bila shaka majadiliano yenye tija kuhusu maamuzi yatakuwa sehemu ya soka siku zote, lakini madai yasiyo na msingi hayana nafasi katika mchezo wetu.
“Hakuna anayeweza kuhoji uadilifu wa maafisa wa mechi za Kombe la Dunia la FIFA. Hali hiyo inapotokea, inaweza kuchochea hisia zinazopelekea kutolewa kwa vitisho dhidi yao na familia zao. Hili si sahihi.”




