World Cup

Serikali Morocco yakana uvumi wa kuikataa Afrika

..yaonya vyombo vya habari vinavyosambaza uzushi huo

RABAT: Serikali ya Morocco imekanusha taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa Waziri wa Michezo, Mohamed Berrada alisema taifa hilo haliiwakilishi Afrika katika Michuano ya Kombe la Dunia na haihitaji uungwaji mkono wa mataifa mengine ya bara hilo.

Katika ufafanuzi uliotolewa na wizara hiyo, Berrada amesema hajawahi kutoa kauli yoyote kwa chombo chochote cha habari kuhusu suala hilo, akibainisha kuwa maneno yanayosambazwa yakihusishwa naye ni ya kubuni na hayawakilishi msimamo wake wala wa Serikali.

Kauli hizo zilianza kusambaa kwa kasi mtandaoni na kuzua mjadala mpana miongoni mwa wadau wa michezo, hasa kutokana na nafasi ya Morocco katika soka la Afrika na dunia.

Wizara hiyo imeeleza kuwa Morocco inaendelea kujivunia utambulisho wake wa Kiafrika na kwamba uhusiano wake wa kihistoria, kiutamaduni na kibinadamu na mataifa mengine ya Afrika ni msingi muhimu wa sera za taifa hilo.

Aidha, vyombo vya habari na watumiaji wa mitandao ya kijamii wametakiwa kuthibitisha ukweli wa taarifa kabla ya kuzisambaza, huku wizara ikisisitiza kuwa itachukua hatua za kisheria dhidi ya watakaobainika kutengeneza au kusambaza taarifa za uongo zinazomhusisha Waziri huyo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button