Namna Wahdzabe walivyofurahia chakula, muziki Zanzibar

ZANZIBAR:JAMII ya Wahadzabe kutoka mkoani Arusha ilikuwa miongoni mwa vivutio vya Tamasha la 29 la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) 2026, ambapo walipata fursa ya kufurahia chakula na burudani ya muziki pamoja na washiriki wengine wa tamasha hilo.
Wahadzabe walihudhuria tamasha hilo sambamba na maonesho ya filamu ya We Are Hadza, inayoangazia maisha, utamaduni na historia ya jamii hiyo ya asili ya Tanzania. Filamu hiyo ilioneshwa kwa mara ya kwanza barani Afrika katika ZIFF 2026
Baada ya maonesho ya filamu, wajumbe wa jamii hiyo walishiriki chakula cha pamoja kilichoandaliwa na waandaaji wa tamasha, huku wakipata nafasi ya kuzungumza na wageni na wadau wa tasnia ya filamu kuhusu utamaduni wao na maisha yao ya kila siku.
Burudani ya muziki na ngoma za asili ilitawala usiku huo, ambapo Wahadzabe walionekana wakicheza na kuimba pamoja na washiriki wengine, jambo lililovutia hadhira na kuonyesha umuhimu wa tamasha hilo katika kuunganisha tamaduni mbalimbali kupitia sanaa.
Washiriki wa tamasha walisema uwepo wa Wahadzabe umeongeza thamani ya ZIFF kwa kuonesha utofauti wa tamaduni za Tanzania na kutoa nafasi kwa jamii za asili kusimulia hadithi zao kupitia filamu.
Filamu ya We Are Hadza inaelezea maisha, mila na changamoto za jamii ya Wahadzabe wanaoishi eneo la Ziwa Eyasi, ikiwa na lengo la kuhifadhi simulizi na urithi wao wa kitamaduni kwa vizazi vijavyo.
ZIFF 2026 iliendelea kutumia filamu, muziki na shughuli za kitamaduni kama njia ya kuunganisha watu kutoka mataifa mbalimbali na kukuza uelewa wa urithi wa Afrika kupitia sanaa.




