Lufingo: Amani ni tunda la haki

MSANII wa filamu, Daniel Lufingo, amesema kuwa uwepo wa amani katika jamii ni jambo muhimu kwa wasanii, kwani kazi zao hutegemea mazingira tulivu pamoja na ushirikiano mzuri kati ya jamii na serikali.
Akizungumza na Spoti Leo, Lufingo maarufu kama “Adam” kutoka tamthilia ya Noma, amesisitiza kuwa amani ya kweli hujengwa juu ya msingi wa haki, ambapo kila mmoja anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa ustawi wa jamii.
“Amani ni tunda la haki. Mtu mmoja anapotimiza wajibu wake kwa mwingine, ndipo amani hupatikana. Huwezi kutenganisha amani na wajibu katika ustawi wa jamii yoyote,” amesema Lufingo.
Ameeleza kuwa bila amani, maendeleo hayawezi kupatikana, hali inayoweza kuathiri sekta mbalimbali ikiwemo sanaa.
“Sisi wasanii tunahitaji jamii kwa sababu ndio wateja wetu, lakini pia tunahitaji mahusiano mazuri na serikali ambayo ni mlezi wetu. Kukosekana kwa amani kunasababisha kazi zetu kusimama na wakati mwingine tunajikuta kwenye njia panda,” ameongeza.
Akizungumzia hali ya sasa ya nchi, Lufingo amesema taifa linaendelea kujijenga upya kufuatia changamoto zilizojitokeza baada ya uchaguzi uliopita wa Oktoba 29, akisisitiza umuhimu wa kila mmoja kutimiza wajibu wake ili kurejesha mshikamano wa kitaifa.
“Kwa sasa nchi inapambana kuponya majeraha ya uchaguzi uliopita, hivyo kila mmoja ana jukumu la kuchangia ujenzi wa upya wa umoja wa kitaifa,” amesema.
Kuhusu nafasi ya vijana, amewahimiza kushiriki kikamilifu katika siasa na shughuli za maendeleo, akibainisha kuwa wao ndio nguvu ya sasa na ya baadaye ya taifa.
“Vijana tuache kusema siasa ni uongo. Siasa ndiyo inaongoza maisha yetu, hivyo tushiriki kikamilifu na tuepuke ubaguzi wa kidini, kikabila au kisiasa ambao ni sumu kwa umoja wetu,” amesema.
Aidha, Lufingo amesema tofauti za kikabila, kidini au kisiasa hazipaswi kuwa kikwazo kwa maendeleo, akieleza kuwa jamii ya sasa ina uelewa mpana zaidi kutokana na elimu.
Ameongeza kuwa wasanii wana wajibu wa kulipa kodi, kuelimisha jamii kupitia kazi zao na kushiriki katika mijadala ya maendeleo.
“Wasanii ni kioo cha jamii na daraja linalounganisha watu. Tunawajibika kuelimisha, kuburudisha na kushauri,” amesema.
Hata hivyo, amekiri kuwa baadhi ya wasanii wanahofia kutoa maoni yao kutokana na changamoto mbalimbali, zikiwemo udhibiti wa maudhui na masuala ya usalama.
Akizungumzia haki za vijana, amesisitiza umuhimu wa kuwapa nafasi ya kusikilizwa na kushirikishwa katika maamuzi ya kitaifa.
“Baadhi ya haki zinaheshimiwa, lakini bado kuna changamoto. Vijana wanahitaji uhuru wa kuzungumza ukweli bila hofu, mradi hawavunji sheria,” amesema.
Amebainisha kuwa njia bora ya kudai haki ni kupitia mazungumzo jumuishi yanayohusisha makundi yote ya jamii.
Kwa upande wake, ameishauri serikali kuendelea kushirikisha wananchi katika maamuzi na kutambua mchango wa wasanii wakati wote, si wakati wa kampeni pekee.
“Serikali itambue kuwa wasanii ni sehemu muhimu ya maendeleo ya taifa, si wakati wa kampeni tu bali wakati wote,” amesisitiza.
Akihitimisha, Lufingo amewataka vijana kudumisha amani kwa kutimiza wajibu wao na kushikamana kwa pamoja.
“Kila mmoja atimize wajibu wake kwa nchi, na nchi itimize wajibu wake kwa raia. Hapo ndipo tutakapopata amani ya kweli,” amehitimisha.




