MUMBAI: INAWEZA kukushangaza lakini ndiyo ukweli muigizaji aliyecheza nafasi ya uandishi wa Habari aliyefuatilia tukio la kuungua kwa treni ya Godhra ya mwaka 2002, Vikran Massey ameweka wazi kwamba amekuwa akipokea vitisho kutokana na ushiriki wake katika tamthilia ya ‘The Sabarmati Report’ yaani Ripoti ya Sabarmati’.
Vikran amesema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa trela ya filamu hiyo huko Mumbai jana Novemba 7, 2024 akidai kwamba amekuwa akipokea vitisho baada ya kujitolea katika mradi huo wa kufichua kilichotokea katika ajali hiyo.
Akizungumzia filamu hiyo Vikran amesema filamu hiyo imeleta majibu ya uchunguzi wa tukio la utata la kuungua kwa treni ya Godhra la mwaka 2002 hivyo amekuwa akipokea jumbe za vitisho bila kujua zinalenga nini kwake.
Vikran amesema filamu hiyo, inayotarajiwa kutolewa mnamo Novemba 15, 2024, inashughulikia matukio ya maisha halisi yanayozunguka kuchomwa moto kwa Sabarmati Express huko Godhra, Gujarat, ambayo yalizua vurugu na machafuko yaliyoenea kote nchini India.
Licha ya mvutano uliozunguka filamu hiyo, muigizaji alibaki thabiti. “Ndiyo, nimepokea vitisho, na kuna uwezekano watanitafuta zaidi “Lakini, kama wasanii, tunasimulia hadithi. Filamu hii inategemea ukweli, na ni jambo ambalo sisi, kama timu, tunashughulikia pamoja. Tutaishughulikia jinsi inavyotakiwa kushughulikiwa.”
Filamu hiyo, iliyoongozwa na Dheeraj Sarna na kutayarishwa na Shobha Kapoor, Ektaa R Kapoor, Amul V Mohan, na Anshul Mohan, inalenga kufichua ukweli wa tukio hilo la kusikitisha. Vikrant anaigiza kama mwandishi wa habari anayechunguza tukio hilo, huku waigizaji pia wanajumuisha Raashii Khanna na Riddhi Dogra, ambao wanaonyesha majukumu muhimu.
‘Ripoti ya Sabarmati’ inaangazia utata na athari iliyoenea ya tukio la Godhra, likilenga kutafuta ukweli wa ajali hiyo huku kukiwa na mivutano ya kisiasa na kijamii.