Muziki

Mshindi wa BSS msimu 16 kujulikana Julai 11

.....kuondoka na Sh milioni 50

DAR ES SALAAM: Mshindi wa fainali ya Mashindano ya Bongo Star Search (BSS) Msimu wa 16 atajinyakulia zawadi ya Sh milioni 50 katika fainali itakayofanyika Julai 11, 2026, kwenye Ukumbi wa Haddypro, Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Spoti LEO, Mkurugenzi wa Benchmark Productions, Ritha Paulsen, amesema maandalizi ya fainali hiyo yamefikia hatua za mwisho, huku waandaaji wakilenga kuandaa tukio lenye viwango vya kimataifa kuanzia uzalishaji hadi matangazo ya moja kwa moja.

“Tunafanya maandalizi ya kina ili kuhakikisha fainali hii inafanyika kwa viwango vya kimataifa katika kila hatua, kuanzia uzalishaji hadi matangazo ya moja kwa moja. Tunataka BSS 16 iwe mfano wa ubora katika sekta ya burudani,” amesema Ritha.

Ameongeza kuwa zawadi ya shilingi milioni 50 imelenga kuwapa motisha washiriki pamoja na kuwawezesha vijana wenye vipaji kujenga taaluma endelevu katika tasnia ya muziki.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Sinema Zetu, Sophia Mgaza, amesema maandalizi ya kiufundi yamekamilika, ikiwemo kuwasili kwa gari maalumu la matangazo ya moja kwa moja (OB Van), ambalo litatumika kurusha fainali hiyo mubashara.

Mgaza amesema ratiba ya maandalizi inaonesha kuwa Julai 8 kutafanyika uwekaji wa vifaa, Julai 9 kutakuwa na mazoezi ya washiriki, bendi na timu ya uzalishaji, huku Julai 10 ikitengwa kwa mazoezi ya mwisho kabla ya fainali ya Julai 11.

Amesisitiza kuwa maandalizi hayo yanalenga kuhakikisha watazamaji wanapata matangazo yenye ubora wa hali ya juu, yanayoendana na kiwango cha uwekezaji uliofanywa katika mashindano hayo.

Mmoja wa washiriki wa BSS Msimu wa 16, Nasra Abubakar, amesema kushiriki katika mashindano hayo tayari kumemfungulia milango ya mafanikio kwa kumpa nafasi ya kuonesha kipaji chake na kujitangaza kwa hadhira kubwa.

Wakati huohuo, Meneja Mwandamizi wa Huduma kwa Vijana wa Benki ya CRDB, Mshindo Magimba, ametangaza kuwa benki hiyo imeingia ubia na Bongo Star Search Msimu wa 16 kwa lengo la kuunga mkono maendeleo ya vijana kupitia elimu ya fedha, mikopo nafuu na fursa za uwekezaji.

Magimba amesema ushirikiano huo ni sehemu ya mkakati wa benki wa kuwekeza katika maendeleo ya vipaji vya vijana kupitia sekta ya burudani. Amebainisha kuwa Bongo Star Search imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kutambua, kukuza na kuwawezesha vijana wenye vipaji nchini Tanzania na hata nje ya mipaka yake.

Related Articles

Back to top button