Furaha’ ya Harmonize yaandika historia

DAR ES SALAAM:WIMBO mpya wa msanii Rajab Abdul ‘Harmonize’, unaojulikana kama Furaha, umeandika historia kwa kuwa wimbo wa kwanza kushika nafasi ya kwanza kwa wakati mmoja kwenye majukwaa yote makubwa ya kusikiliza muziki mwaka huu wa 2025.
Ndani ya siku nne tangu kutolewa, Furaha imefika namba moja kwenye majukwaa ya Apple Music, Audiomack, YouTube Music, na pia kuwa wimbo unaotafutwa zaidi kwenye Boomplay.
Hii ni rekodi kubwa kwa Harmonize, ikiimarisha nafasi yake kama mmoja wa wasanii wenye ushawishi mkubwa kwenye muziki wa Bongo Fleva.
Kwa utayarishaji wa Kimambo Beats, Furaha si tu wimbo wa mapenzi, bali pia unatoa ujumbe wa kutafakari juu ya furaha ya kweli, jambo linaloonekana kuwagusa mashabiki wengi.
Kwa mafanikio haya, Harmonize anazidi kuthibitisha ubora wake katika historia ya muziki wa Tanzania.




