Mpanzu ‘Volkano’ kulipuka Dabi ya Kariakoo

DAR ES SALAAM: Kadri inavyokaribia mechi ya Dabi ya Kariakoo Jumamosi, Machi 8, kasi na madhara ya kiungo mshambuliaji wa Simba, Elie Mpanzu, yanafananishwa na mlipuko wa volkano—nguvu isiyozuilika inapotokea.
Nyota huyo anatarajiwa kuonesha uwezo wake katika mchezo huo, ikiwa ni mechi yake ya kwanza kucheza katika Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga, uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesisitiza kuwa Mpanzu si tu mchezaji mwenye kasi ya ajabu, bali pia ana maamuzi ya haraka na uwezo mkubwa wa kuvuruga ngome za wapinzani.
“Mpanzu hana hofu ya kushambulia moja kwa moja. Kila anaposhika mpira, lengo lake ni moja—kuhakikisha timu yake inapata bao,” amesema Ahmed.
Kwa mujibu wa Ahmed, kabla ya kutaja ubora wa wachezaji kama Leonel Ateba na Steven Mukwala, ni muhimu kwanza kutambua mchango mkubwa wa Mpanzu, ambaye kwa sasa ndiye mhimili wa mabao ndani ya kikosi cha Simba.
Kwa mashabiki wa Simba, jina “Volcano” linazidi kupata maana halisi, likionyesha kuwa timu yao ina mchezaji ambaye anawatia hofu wapinzani, kama mlipuko wa volcano usioweza kuzuilika.