Masau aita mashabiki kuiunga mkono JKT

DAR ES SALAAM: OFISA Habari wa JKT Tanzania, Masau Bwire, amesema kikosi hicho kimejipanga kupata ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba FC ya Mwanza, utakaochezwa Septemba 5, katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Aidha, amewataka mashabiki wa JKT Tanzania na wakazi wa Mwembeni kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kuwapa nguvu wachezaji, akisisitiza kuwa lengo lao ni kuvuna pointi tatu dhidi ya Pamba FC.
Bwire amesema mchezo huo una umuhimu mkubwa kwa JKT Tanzania katika kusogea juu kwenye msimamo wa ligi, huku akisisitiza kuwa wanatambua Pamba ni timu yenye ushindani na hivyo hawataingia uwanjani kwa kuibeza.
Amesema kikosi chao kiko tayari kwa mchezo huo bila kuwa na majeruhi wala wagonjwa, hivyo benchi la ufundi litakuwa na jukumu la kuchagua kikosi kitakachoanza.
“Ni mchezo ambao sisi tumeupa uzito na umuhimu mkubwa. Tunahitaji utusogeze hatua kadhaa kwenda juu kileleni. Tunajiamini katika uwezo wetu, maandalizi yetu na uwezo wa kikosi chetu. Vijana wetu wote wako tayari, hatuna majeruhi wala mgonjwa, hivyo tunatarajia kuvuna alama tatu kutoka kwa Pamba FC ya Mwanza.”amesema.
JKT Tanzania ina pointi nne baada ya mechi nne, huku Pamba ikiwa na pointi moja.




