Mitindo

Miss Tanzania yakabidhiwa Lamata Village

DAR ES SALAAM. MASHINDANO ya urembo ya Miss Tanzania yameingia katika sura mpya baada ya jukumu la kuyaendesha kukabidhiwa rasmi kwa taasisi ya Lamata Village, hatua inayotarajiwa kurejesha hadhi na mvuto wa shindano hilo lenye historia kubwa nchini.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo Leo Aprili 14, mwaka huu, Mkurugenzi wa Kampuni ya The Look, Basila Mwanukuzi amesema tangu kuanzishwa kwake mwaka 1994, Miss Tanzania imekuwa chachu ya mabadiliko kwa washiriki wake na jamii kwa ujumla.

Amesema kuwa washindi wengi waliopita wamefanikiwa kuwa na ushawishi mkubwa katika nyanja mbalimbali, huku baadhi yao wakijikita kwenye tasnia ya sanaa ikiwemo uigizaji, akiwataja majina kama Jokate Mwegelo na Aunt Ezekiel.

“Ukifuatilia historia ya Miss Tanzania kuanzia mwaka 1994 hadi sasa, utaona namna ambavyo washindi wake wamekuwa na mchango mkubwa katika jamii. Wamekuwa zaidi ya warembo, ni watu wenye ushawishi na dira,” amesema.

Amebainisha kuwa baada ya kuongoza kwa muda mrefu, walifikia wakati wa kuachia nafasi hiyo kwa kizazi kipya chenye mawazo mapya na ubunifu zaidi.

“Nilijiuliza namwachia nani jukumu hili. Tulihitaji changamoto mpya, watu wenye nguvu mpya na maono mapya. Ndipo tukafikia uamuzi wa kukabidhi kwa Lamata Village, ambao historia yao inaeleweka na uwezo wao unaonekana,” ameongeza.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Lamata Village, Grace Mgaya, amesema wanapokea jukumu hilo kwa uzito mkubwa huku wakiahidi kuleta mageuzi chanya katika mashindano hayo.

“Tunapokea jukumu hili kwa mikono miwili na kwa uzito wake. Tunatambua dhamana tuliyopewa na tunaahidi kuisimamia kwa weledi mkubwa,” amesema.

“Lamata siyo tu waandaaji wa shindano, bali ni taasisi yenye dira ya kumjenga mtu. Tunataka kurejesha hadhi ya Miss Tanzania kama ilivyokuwa zamani na hata zaidi,” ameongeza.

Grace Mgaya pia alitoa wito kwa wadau mbalimbali wa tasnia ya urembo wakiwemo wakala na wadhamini kujitokeza kushirikiana nao, akisisitiza kuwa milango iko wazi kwa ushirikiano.

Katika hatua nyingine, amesema maandalizi ya uzinduzi rasmi wa mashindano hayo yanaendelea, huku wakipanga kuanza na mkataba wa miaka mitatu wa utekelezaji wa mradi huo.

Naye Lea Mwendamseke Lamata, ambaye ni Mkurugenzi wa Lamata Village amesema ana matumaini makubwa na mwelekeo mpya wa mashindano hayo, akieleza kuwa anaamini ubora utaendelea kupewa kipaumbele.

“Mashindano haya nayapenda na naamini yatakuwa bora zaidi. Kilicho muhimu ni kuhakikisha tunapata washindi wenye viwango na maadili,” alisema.

Kwa upande wake, Ofisa Sanaa Mwandamizi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Abel Ndaga, amesisitiza kuwa mashindano ya Miss Tanzania hayapaswi kuchukuliwa kama ya urembo pekee, bali ni jukwaa la kuibua viongozi wa baadaye.

“Miss Tanzania siyo urembo tu. Ni jukwaa ambalo limezalisha viongozi na watu wenye mchango mkubwa katika taifa. BASATA tuko tayari kutoa ushirikiano kuhakikisha mashindano yanaendeshwa kwa weledi na kufuata taratibu,” amesema.

 

Related Articles

Back to top button