Hamisa avujisha faili la kutoboa kimaisha
MWANAMITINDO, Hamisa Mobetto ameshinda tuzo ya balozi bora Afrika katika tuzo za 100 Best Brand Africa na kudai kuwa mtindo wake wa maisha, kujituma na hamu ya mafanikio ndio siri ya kupata tuzo hiyo.
Hamisa amesema kuwa nidhamu na unyenyekevu ndicho kinachomtofautisha na wasanii wengine.
Kupitia ukurasa wake wake wa Instagram Hamisa amechapisha ujumbe huo na kutoa shukrani kwa kupewa tuzo ya msanii anayeongoza kuwa balozi wa bidhaa mbalimbali.
Amesema juhudi zake katika kazi zimemwezesha kupata tuzo hiyo ya balozi bora katika The 100 Best Brands Africa.
‘’Nina furaha na shukrani zisizo na kipimo! kushinda tuzo ya balozi wa bidhaa (Brand Ambassador Bora) wa mwaka katika The 100 Best Brands Africa ni uthibitisho kwamba unyenyekevu, kujituma, na hamu ya kukua ndio msingi wa mafanikio.
‘’Kila hatua ninayochukua inaendeshwa na shauku ya kuwa bora zaidi, kuwa na nguvu zaidi, na kuvuka mipaka.
Asanteni kwa wote wanaoamini katika safari yangu ya mafanikio’’ameandika Hamisa Mobetto.