Messi ‘fiti’ kuwavaa FC Porto

ATLANTA: KOCHA wa Inter Miami, Javier Mascherano amesema staa wa klabu hiyo raia wa Argentina Lionel Messi atakuwa ‘fiti’ kuwavaa FC Porto ya Ureno katika mchezo wa Kombe la Dunia la Klabu baadae leo Alhamisi licha ya kuonesha dalili za maumivu baada ya kuonekana akishika mguu wa kushoto na kuchechemea mazoezini.
Video iliibuka kwenye mitandao ya kijamii ikionesha Messi akigusa mguu wake wa kushoto na kuchechemea wakati wa mazoezi jana Jumatano lakini kocha wake Mascherano amethibitisha kuwa fowadi huyo mkongwe atakuwa tayari kwa mechi ya pili ya Kundi A ya Inter Miami jijini Atlanta.
“Nikiwa safarini kutoka Miami kuja Atlanta niliona hiyo (video) sehemu fulani, lakini Messi yuko fiti, amefanya mazoezi, amemaliza ‘session’ nzima. Alikuwa akigusa mguu wake ndio, wakati mwingine watu wanajigusa sehemu mbalimbali za miili yao, lakini hakuna shida, yuko fiti na ni wazi atacheza kesho.” Mascherano amewaambia waandishi wa habari.
Kocha huyo pia alisema mchezaji mwenzake wa zamani wa Barcelona, Jordi Alba, atapatikana katika mchezo huo baada ya kukosa mechi ya ufunguzi ya 0-0 dhidi ya Al Ahly kutokana na majeraha.
Wakati huohuo Mascherano amesema kumiliki mpira ni nguzo yake muhimu kuelekea mchezo wake dhidi ya FC Porto ya Ureno utakaopigwa majira ya saa 4 usiku saa za Afrika Mashariki. Porto ni washiriki wa mara kwa mara wa Ligi ya Mabingwa Ulaya jambo ambalo linatarajia kuwapa mtihani mkubwa timu hiyo ya MLS.




