Mastaa waliostaafu soka 2024

KILA msimu wa mpira wa miguu unapoisha, tunakutana na furaha ya ubingwa kwa timu tofauti tofauti,tuzo za wachezaji na majonzi ya kuwaaga wachezaji waliotupa burudani kwa miaka mingi.
Mwaka 2024, mambo yamekuwa vilevile, ulimwengu wa soka ulipoteza baadhi ya nyota wake wakubwa baada ya kutangaza kustaafu.Kikubwa ni kwamba wachezaji hao wametuachia urithi wa kumbukumbu za ushindi, vipaji vya kipekee, na shangwe zisizosahaulika.
Katika makala hii, tunawapigia saluti baadhi ya wachezaji wa mpira wa miguu waliostaafu mwaka huu wa 2024 huku tukichunguza maisha yao ya uwanjani, klabu walizochezea, na rekodi walizovunja.
ANDRES INIESTA (2002-2024)
Mwanasoka huyu wa Kihispania alikuwa kiongozi wa uwanja kwa utulivu na akili yake ya mpira. Iniesta alijulikana kwa uwezo wake wa kutoa pasi sahihi na kufanikisha mashambulizi.Viungo Xavi Hernandez na Sergio Busquets walitengeneza kombinesheni matata sana ukimjumlisha na Iniesta pale dimba la kati.
Iniesta ni zao maalumu la La Masia ambapo baada ya kuhitimu vyema akaanza kuitumikia Barcelona ya wakubwa mnamo Oktoba 29 mwaka 2002 akiwa na miaka 18 tu katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Club Brugge. Baada ya hapo, kila kitu kikabaki kuwa historia kwani gwiji huyu alikwenda kuichezea Barcelona kwa misimu 16, akicheza jumla ya michezo 674 na kufunga mabao 57 pamoja na pasi 135 za mabao.
Akiwa na Barcelona, Iniesta alishinda La Liga mara 9, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara 4, Kombe la dunia la klabu mara 3, Copa Del Rey mara 6 na Kombe la Super Cup Ulaya mara 4. Baada ya hapo akatimkia zake Japan ili tu asipate nafasi yoyote ya kucheza dhidi ya timu yake pendwa ya Barcelona, na huko akatua katika klabu ya Vissel Kobe ambapo ameichezea michezo 134, akifunga mabao 26 na pasi 25 za mabao. Katika timu ya taifa, umuhimu wa Iniesta ni mkubwa sana katika kikosi chao cha dhahabu na Iniesta atakumbukwa kwa kufunga bao la pekee na la ushindi kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2010 dhidi ya Uholanzi na kutwaa taji hilo. Pia Iniesta alishinda mataji mawili mfululizo ya Euro na Hispania mwaka 2008 na mwaka 2012.
TONI KROOS (2007-2024)
Wengi walipenda kumuita ‘The German Sniper’ kutokana na uhodari wake wa kuona mbali katika dimba na kutoa pasi kwa usahihi katika maeneo hayo na pia kwa yale mashuti yake makali yaliyotetemesha nyavu za magolikipa wengi. Kutoka Bundesliga hadi La Liga, Kroos alikuwa daraja la juu katika kila klabu zote alizochezea. Kroos amecheza katika klabu za Klabu za Bayer Leverkusen (mkopo), Bayern Munich (2007–2014), na Real Madrid (2014–2024).
Huyu ndiye mjerumani mwenye mataji mengi zaidi kuliko yeyote, ametwaa mataji 34 katika kazi yake ya soka aliyoitumikia kwa zaidi ya miaka 17. Akiwa na Real Madrid, Kroos amebeba mataji 21.
Toni Kroos amecheza michezo zaidi ya 750 akifunga mabao zaidi ya 80 na kutoa pasi zaidi ya 180 za mabao. Kroos ameichezea timu ya taifa ya Ujerumani mara 114 na kiwango chake bora kiliisadia timu hiyo kutwaa Kombe la Dunia 2014.
THIAGO ALCANTARA (2008-2024)
Thiago Alcântara alisimama kama kiungo mwenye uwezo wa kuchanganya burudani na ufanisi wa mchezo. Akiwa mtoto wa mchezaji wa zamani Mazinho, Thiago alirithi damu ya soka.Alikuwa mtaalamu wa kuunda nafasi kwa njia za kiufundi na ubunifu wa hali ya juu.vijana wengi waliokuwa wanatamani kucheza nafasi ya kiungo, walimtazama Thiago kama kioo chao cha kujifunza mbiu,kujiamini ukiwa na burudani na jicho la kuutazama uwanja.
Thiago aliichezea Barcelona kuanzia 2009 hadi 2013, kisha akahamia Bayern Munich 2013 hadi 2020 na kisha kuhitimisha safari yake nchini England akiwa na Liverpool mwaka 2020 hadi 2024 alipostaafu.
Thiago amecheza michezo zaidi ya 480 ya klabu akifunga mabao zaidi ya 40 na pasi zaidi ya 60 za mabao.Kutokana na uwezo wake mkubwa na klabu zenye hadhi alizochezea, Thiago ameshinda mataji 11 ya Ligi Kuu, yakiwemo Bundesliga mara 7 na EPL mara 1. Pia ameshinda mataji mawili ya Ligi ya Mbaingwa Ulaya,mataji mawili ya kombe la dunia la klabu,taji 1 la FA na mataji mengine.
RAPHAEL VARANE (2010-2024)
Raphaël Varane ni mlinzi wa kizazi kipya aliyekamilika kwa kasi, nguvu, na uwezo wa kusoma mchezo. Alikuwa tegemeo kwenye timu zote alizochezea. Varane alitofautiana sana na mabeki wengine wengi kwani yeye hakutegemea tua nguvu au kasi yake aliyokuwa nayo bali yeye alionesha utulivu wa hali ya juu wa akili pamoja na uwezo mkubwa wa kuusoma mchezo hali iliyomsaidia kuzuia mashambulizi kabla hata ya hatari kufika.
Akiwa na urefu wa futi 6 na inchi 3 (1.91m) Varane alitawala mipira ya juu katika maeneo hatari na hii ilimsaidia pia kupambana na washambuliaji wenye nguvu za kimwili.
Varane amechezea Lens (2010–2011), Real Madrid (2011–2021) na Manchester United (2021–2024).
Pia ni mmoja ya wachezaji wenye mafanikio makubwa katika soka akifanikiwa kutwaa mataji manne ya Ligi ya Mabingwa, La Liga mara 3, Kombe la FA mara 1 na Kombe la Dunia mwaka 2018 akiwa na Ufaransa.Mara nyingine ukifanikiwa sana, unakuwa huna sababu nyingine ya kuendelea kufanya unachokifanya, Varane amestaafu soka akiwa na umri wa miaka 31 tu.
PEPE (2001-2024)
Pepe alikuwa kiongozi wa safu ya ulinzi, mwenye ukakamavu na roho ya kupambana. Alijulikana kwa uwezo wake wa kuondoa hatari na kuwanyamazisha washambuliaji hatari.
Pepe, jina halisi likiwa ni Képler Laveran de Lima Ferreira,alikuwa na sifa za ziadi zilizomfanya kuwa zaidi ya beki hii ni kutokana na uwezo wa kujituma kwa ajili ya timu,alikuwa ni mlinzi asiyeogopa chochote wala yeyote, lakini kikubwa zaidi alikuwa ni kiongozi ndani na nje ya uwanjani hata kama hakuwa nahodha kwa wakati huo.
Pepe amecheza katika klabu za Marítimo, Porto, Real Madrid na Beşiktaş. Hadi anastaafu katika kazi hiyo iliyodumu kwa takribani miaka 23, Pepe amecheza zaidi ya michezo 750 akifanikiwa kufunga mabao yanayokaribia 50 licha ya nafasi yake ya ulinzi. Pepe ameshinda mataji yapatayo 34.
Majina yalikuwa mengi lakini SpotiLeo tumekuchagulia hayo makubwa na tuyanaamini walikupa burudani katika enzi zao za kucheza soka.
Wengine waliostaafu mwaka 2024 ni Leonardo Bonucci (2005-2024) Marouane Fellaini (2006-2024) Joe Hart (2003-2024), Luis Nani, Joel Matip,Cladio Bravo,Phil Jones,Ryan Bertrand na Shkodran Mustafi. Tusubiri 2025, tuone ni kina nani tutawapigia saluti tena kwa kazi kubwa waliyoifanya miaka ya nyuma katika soka.