Nyumbani

Mchezo wa rugby wapata msukumo mpya Tanzania

DAR ES SALAAM: Kampuni ya SportPesa imeingia ushirikiano na Tanzania Rugby Union (TRU) kwa ajili ya kuendeleza na kukuza mchezo wa rugby nchini Tanzania, huku kampuni hiyo ikiwa Mdhamini Mkuu wa Mashindano ya Taifa ya Rugby Saba yatakayojulikana kama SportPesa National Saba Circuit 2026.

Ushirikiano huo wa miezi mitano pia utaifanya SportPesa kuwa Mshirika Rasmi wa Kipekee wa Kamari wa mashindano hayo, huku ikiwekeza katika kuongeza mwonekano wa mashindano, ushirikishwaji wa mashabiki, maudhui ya kidijitali, shughuli za uwanjani pamoja na programu za kuendeleza vipaji vya rugby.

Akizungumza wakati wa kutangaza ushirikiano huo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa SportPesa Tanzania, Tracy Humplick, amesema kampuni hiyo inaamini uwekezaji ni muhimu katika kujenga sekta imara ya michezo na kwamba rugby ina nafasi kubwa ya kukua nchini Tanzania.

Amesema uzoefu wa SportPesa katika kuunga mkono rugby nchini Kenya na Afrika Kusini umeongeza imani ya kampuni hiyo kwamba inaweza kuchangia maendeleo ya mchezo huo Tanzania.

Kwa upande wake, Rais wa Tanzania Rugby Union, Jacob Jonas, amesema ushirikiano huo umefika wakati muhimu kwa maendeleo ya rugby nchini, kwani utasaidia kuimarisha Mashindano ya Taifa ya Rugby Saba na kutoa fursa zaidi kwa wachezaji, makocha na vipaji chipukizi.

Amesema msisitizo uliowekwa katika maendeleo ya mchezo na ushirikishwaji wa mashabiki ni muhimu katika kujenga jamii kubwa inayounga mkono rugby.

Mbali na Mashindano ya Taifa ya Rugby Saba na Timu ya Taifa ya Wanaume, ushirikiano huo utaisaidia pia Twiga Kingskatika safari yake ya kwenda Afrika Kusini kushiriki mashindano ya Obaro 7s yanayotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Hatua ya kwanza ya ushirikiano huo itaonekana kupitia Dar Rugby Saba 2026, inayotarajiwa kufanyika Agosti 29 katika Uwanja wa Leaders Club, Dar es Salaam.

Dar Rugby Saba 2026 ni hatua ya pili ya SportPesa National Saba Circuit 2026, ambapo zaidi ya timu 10 kutoka mikoa mbalimbali zinatarajiwa kushiriki na kukusanya pointi muhimu kuelekea Grand Finale itakayofanyika baadaye mwaka huu.

Mashindano hayo pia yatahusisha timu za wanawake, huku mashabiki na wananchi wakialikwa kufika uwanjani kushuhudia mashindano na kuziunga mkono timu zitakazoshiriki.

Kabla ya mashindano hayo, SportPesa na TRU zitaendesha shughuli za maendeleo ya rugby zitakazomhusisha Robert Bwali, Game Growth Manager, Eastern and Southern Africa kutoka Rugby Afrique, ambaye atatembelea timu katika maeneo yao ya mazoezi na kutoa maarifa ya kiufundi kwa wachezaji wakati wa maandalizi ya mwisho kuelekea siku ya mashindano.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button