Ligi KuuNyumbani

Yanga hesabu kwa Azam, Zalan

TIMU ya Yanga imeanza rasmi mazoezi ya maandalizi ya mechi yao dhidi ya zam, huku pia ikijiwinda dhidi ya wapinzani wake wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Zalan ya Sudan.

Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara walikuwa na mapumziko ya siku mbili baada ya kurejea Agosti 21 kutoka Arusha ilikoshinda mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union na sasa imeanza kujiweka sawa kwa ajili ya mechi hizo.

Timu hiyo itaumana na Azam Septemba 6 kwenye Uwanja wa Mkapa kabla ya kupepetana na Zalan kwenye mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika Septemba 10, 2022.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Meneja wa Yanga, Walter Harrison ameliambia gazeti la HabariLEO kuwa kuna uwezekano mkubwa mechi yao ya ugenini dhidi ya Zalan ikapigwa kwa Mkapa baada ya uwepo wa maombi hayo kutoka kwa uongozi wa timu hiyo.

“Bado sijapata hizi taarifa kwa maelezo ya kutosha, lakini nilichoelekezwa mpaka sasa ni kwamba kuna maombi ya namna hiyo kutokana na sababu mbalimbali na wao wamechagua kucheza hapa mchezo wao wa nyumbani.

“Lakini kwa ujumla maandalizi yameanza leo (jana) dhidi ya michezo hiyo miwili, wa Azam na Zalan maana mechi hizi zinapishana kwa siku tatu tu hivi na kama kocha atahitaji mechi
za kirafiki hivi karibuni kabla ya kucheza na wapinzani wetu basi itawekwa wazi,” alisema Harrison.

Harrison pia aligusia ugumu wa mchezo wao na Azam akieleza kuwa wanafahamu  amesajili  vizuri na wameanza vyema ligi na wao wanalitambua hilo, ndiyo maana wapo kwenye maandalizi kabambe ya kuhakikisha wanapata ushindi siku hiyo.

Azam inashikilia nafasi ya tano ikiwa na pointi nne baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar na sare ya 1-1 dhidi ya Geita Gold wakati Yanga ikishikilia nafasi ya pili baada ya kukusanya pointi sita kutoka kwa Coastal na kuibamiza Polisi Tanzania mabao 2-1.

Related Articles

Back to top button