Filamu mpya zitakazotikisa mwaka 2026

MSIMU wa mwisho wa mwaka 2026 unatarajiwa kuwa na burudani kubwa kwa mashabiki wa filamu, huku Hollywood ikijiandaa kuachia filamu kadhaa zinazotarajiwa kuvuta hisia za watazamaji duniani.
Miongoni mwa filamu hizo ni ‘Practical Magic 2’, ‘Resident Evil’ na ‘The Hunger Games: Sunrise on the Reaping’.
‘Practical Magic 2’ ni miongoni mwa filamu zinazotajwa kuwa na mvuto mkubwa, hasa kutokana na kurejea kwa hadithi ya familia ya Owens inayohusisha uchawi. Filamu hiyo imepangwa kuingia katika kumbi za sinema Septemba 11, 2026.
Kwa upande wa filamu za kutisha, ‘Resident Evil’ inatarajiwa kurejea kwenye skrini kupitia toleo jipya linaloongozwa na Zach Cregger. Filamu hiyo inatarajiwa kuachiwa Septemba 18, 2026, huku Austin Abrams akiwa miongoni mwa waigizaji wakuu.
Mashabiki wa ‘The Hunger Games’ nao wanatarajia sura mpya kupitia Sunrise on the Reaping, inayosimulia hadithi inayohusisha mashindano ya Haymitch Abernathy. Filamu hiyo imepangwa kutoka Novemba 20, 2026, ikiwa na waigizaji kama Joseph Zada, Elle Fanning na Ralph Fiennes.
Filamu nyingine inayotarajiwa kuteka hisia za mashabiki ni ‘Godzilla Minus Zero’, ambayo inamrudisha tena Godzilla kwenye skrini katika simulizi jipya. Filamu hiyo imepangwa kuoneshwa nchini Japan Novemba 3 na Amerika Kaskazini Novemba 6, 2026.
Kwa ujumla, ratiba ya mwisho wa mwaka inaonekana kuwa na ushindani mkubwa, huku filamu za aina mbalimbali zikitarajiwa kukutana katika kumbi za sinema. Mbali na filamu hizo, ‘Avengers: Doomsday’ na ‘Dune: Part Three’ pia ni miongoni mwa majina makubwa yanayotarajiwa kuhitimisha mwaka 2026 kwa burudani kubwa




