Filamu

Taylor Sheridan ashitakiwa kunakili wazo la Yellowstone

MAREKANI: Mtayarishaji na mwandishi wa mfululizo maarufu wa televisheni ‘Yellowstone’, Taylor Sheridan, anakabiliwa na kesi ya madai ya ukiukaji wa hakimiliki baada ya mwandishi Lauren J. Salkin kumshutumu kutumia wazo lake katika kutengeneza mfululizo huo.

Kesi hiyo imefunguliwa katika mahakama ya shirikisho nchini Marekani.

Salkin anadai kuwa mwaka 2016 aliandaa mradi wa televisheni uliokuwa ukiitwa ‘Sovereign Nation’, ambao ulihusisha masuala ya utawala wa makabila, migogoro ya ardhi, maendeleo na nguvu za kiuchumi zinazohusiana na kasino.

Kwa mujibu wa madai yaliyowasilishwa mahakamani, Salkin anasema aliwasilisha kwa wawakilishi wa Sheridan script ya kipindi cha majaribio, show bible pamoja na pitch deck mwishoni mwa mwaka 2016 na mwanzoni mwa 2017. Anadai kuwa baadaye aliarifiwa kuwa Sheridan hakuwa akipokea miradi ya televisheni.

Mwandishi huyo anadai kuwa miezi michache baadaye, Yellowstone iliidhinishwa na kuanza kuonekana kwenye televisheni mwaka 2018, huku akidai kuwa kuna mfanano mkubwa kati ya kazi yake na mfululizo huo, ikiwemo mada, wahusika na migogoro inayohusu ardhi.

Related Articles

Back to top button