Kifo cha mzee Said Kibore, gumzo mitandaoni

DAR ES SALAAM: Tanzania imepata pigo katika tasnia ya burudani kufuatia kifo cha Mzee Said Kibore, msanii na mwigizaji aliyepata umaarufu mkubwa mitandaoni kupitia video zake zilizokuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Kibore alijizolea umaarufu zaidi baada ya video yake akiimba kwa hisia wimbo ‘Nisamehe’, maarufu kama ‘Fala’, akimzungumzia binti aliyemsaliti kusambaa kwa kasi na kuvutia hisia za watu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.
Mbali na umaarufu alioupata kupitia mitandao ya kijamii, Mzee Said Kibore alifahamika pia kama mwigizaji na msanii wa maudhui, akitumia ucheshi na ubunifu wake kuwaburudisha mashabiki.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari, Kibore aliugua ghafla akiwa nyumbani jijini Dar es Salaam tarehe 22 Agosti 2026, kabla ya kupelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa jitihada za matibabu hazikuweza kuokoa maisha yake, huku msiba wake ukiwaacha mashabiki, ndugu na wadau wa burudani nchini Tanzania wakiwa katika majonzi wakati walipompumzisha kwenye nyumba yake ya milele jana.
Mzee Said Kibore amefariki akiwa ameacha kumbukumbu kubwa kwa mashabiki waliomfahamu kupitia kazi zake na hasa video iliyomfanya kuwa gumzo mitandaoni, huku kifo chake kikiendelea kuibua maombolezo katika mitandao ya kijamii.




