Nyumbani

Prisons, Best Six, Tai mabingwa wavu Dar

DAR ES SALAAM: TIMU za Jeshi Stars, Tanzania Prisons, Best Six na Tai zimetawazwa mabingwa wa Ligi ya Mpira wa Wavu Mkoa wa Dar es Salaam (DAREVA) kwa msimu wa 2026 katika makundi ya Seria A na Seria B.

Katika Seria A, Jeshi Stars ilitwaa ubingwa wa wanaume huku Tanzania Prisons ikitwaa ubingwa wa wanawake. Kwa upande wa Seria B, Best Six iliibuka bingwa wa wanaume na Tai ikatwaa ubingwa wa wanawake.

Jeshi Stars ilitwaa taji la Seria A baada ya kuifunga Tanzania Prisons kwa seti 3-1 katika mchezo wa fainali ya wanaume. Kwa wanawake wa Seria A, Tanzania Prisons iliichapa Chui kwa seti 3-1. Iliyomalizika Jana kwenye viwanja vya Kampala Gongolamboto.

Katika Seria B, Best Six iliichapa TPDC kwa seti 3-0 na kutwaa ubingwa wa wanaume, huku Tai ikiwashinda Nyika kwa seti 3-2 na kutwaa ubingwa wa wanawake.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa ligi hiyo, mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa Smart Sport, George Wakuganda, amesema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na DAREVA katika kuendeleza mchezo wa mpira wa wavu.

“Tutashirikiana na wadhamini wengine kuhakikisha tunasaidia kuendesha gurudumu la maendeleo ya mpira wa wavu. Katika mashindano yajayo, Smart Sport itatoa seti za jezi kwa kila timu itakayoshiriki,” amesema Wakuganda.

Kocha wa Jeshi Stars, Zainabu Thabiti, amesema ushindi huo umetokana na maandalizi mazuri, nidhamu ya wachezaji na ushirikiano wa viongozi wa timu.

“Huu ni mwendelezo wa ushindi wetu. Tunamshukuru Mungu na tunaomba atuongoze ili tuendelee kufanya vizuri katika mashindano mengine,” amesema.

Kwa upande wake, Kocha wa Tanzania Prisons, Dismas Dick, amesema safari ya kutwaa ubingwa haikuwa rahisi kwani walipoteza mchezo mmoja katika hatua ya mtoano kabla ya kushinda michezo iliyofuata na kutwaa taji.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button