Ceferin amshangaza Infantino, akataa kugombea

Rais wa UEFA, Aleksander Čeferin, amesema hana mpango wa kugombea nafasi ya urais wa FIFA dhidi ya Gianni Infantino katika uchaguzi ujao, licha ya kuongezeka kwa presha dhidi ya rais huyo wa FIFA.
Čeferin amesema hataki kuchukua nafasi ya Infantino kwa sababu anaendelea kufurahia kazi yake ndani ya UEFA, huku akieleza kuwa kutokuwa na nia ya kugombea urais wa FIFA kunamsaidia pia kudumisha uaminifu wake kama mkosoaji wa baadhi ya maamuzi ya Infantino.
Hata hivyo, Čeferin ametoa onyo kwa Infantino akisema iwapo ataamua kugombea tena katika uchaguzi wa FIFA unaotarajiwa Machi 2027, kuna uwezekano mkubwa wa kukutana na mpinzani. Amesema Infantino anaweza kuchagua kujiuzulu au kwenda kwenye uchaguzi na kukabiliana na mgombea mwingine.
Kauli hiyo imekuja baada ya Infantino kukumbwa na upinzani kuhusu mpango wake uliotelekezwa wa kutafuta uwekezaji binafsi katika mashindano ya FIFA, ikiwemo Kombe la Dunia. UEFA na baadhi ya mashirikisho mengine yameonyesha upinzani dhidi ya mpango huo.
Čeferin pia amekosoa vikali mpango huo, akieleza kuwa ulikuwa tishio kubwa kwa soka na akilinganisha uzito wake na mpango wa European Super League uliopingwa na UEFA miaka iliyopita. Wakati huo huo, majina kama Victor Montagliani wa CONCACAF na Sheikh Salman bin Ebrahim al-Khalifa wa AFC yanatajwa miongoni mwa watu wanaoweza kuibuka kama wapinzani wa Infantino.




