Norway yapokelewa kwa shwange na vifijo

OSLO: Licha ya kutolewa kwenye robo fainali ya Kombe la Dunia 2026, timu ya taifa ya Norway imepokelewa kwa shangwe kubwa nyumbani, huku zaidi ya mashabiki 100,000 wakifurika mitaa ya jiji la Oslo kuwapongeza wachezaji kwa safari yao ya kihistoria.
Norway iliondolewa na England kwa kufungwa mabao 2-1 baada ya muda wa nyongeza, lakini hilo halikuwazuia wananchi kuandaa mapokezi makubwa kwa kikosi hicho kilichofika hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo.
Kikosi hicho kilipokelewa kwa saluti ya maji kutoka kwa zimamoto baada ya kutua Oslo, kabla ya kuanza gwaride la wazi kuelekea Ikulu ya Kifalme, ambako kilikutana na Mfalme Harald. Maelfu ya mashabiki walijaza eneo la ikulu na barabara kuu ya Karl Johans Gate wakipeperusha bendera na kuimba nyimbo za kuisifu timu yao.
Kocha wa Norway, Stale Solbakken, amesema mshambuliaji Erling Haaland na kiungo Sander Berge walilazimika kuondoka mapema ili kuwahi safari za ndege baada ya kuchelewa kwa safari yao kutoka Marekani, hivyo Haaland hakushiriki sehemu ya mwisho ya sherehe hizo.
Gwaride hilo lilikumbana na changamoto baada ya basi la wazi walilokuwa wamepanda wachezaji kusimama kwa muda kutokana na nyaya zilizokuwa zimeshuka chini, na kuwalazimu wachezaji kukaa chini kabla ya safari kuendelea.
Nahodha Martin Odegaard amesema mapokezi hayo yamezidi matarajio yao, akiwashukuru mashabiki kwa sapoti waliyoitoa nchini Marekani wakati wa Kombe la Dunia na walivyoendelea kuionesha waliporejea nyumbani.
Ingawa ndoto ya kutwaa Kombe la Dunia ilisitishwa na England, wananchi wa Norway wameonesha kuwa mafanikio ya timu yao yamekuwa chanzo cha fahari kubwa kwa taifa hilo na wamewapongeza wachezaji wao kama mabingwa.




