AFCON

Makonda: AFCON na Miss World ni fursa za biashara nchini

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amewataka Watanzania kujiandaa kutumia matukio makubwa yanayotarajiwa kufanyika nchini, ikiwemo michuano ya AFCON na mashindano ya Miss World, kama fursa za kufanya biashara, kujiongezea kipato na kukuza uchumi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa msimu wa nne wa kipindi cha CRDB Zogo Mchongo katika makao makuu ya Benki ya CRDB, Makonda alisema matukio hayo yatafungua fursa nyingi za kiuchumi ambazo Watanzania wanapaswa kujiandaa kuzitumia.

“Matumizi ya watu wenye ushawishi mkubwa katika jamii kama wasanii, watengeneza maudhui kuhamasisha elimu ya fedha yanasaidia kuongeza uelewa wa fursa za kiuchumi, kuchochea ajira na kuongeza kipato kwa vijana wanaotumia vipaji vyao kutengeneza maudhui.”

Amesema mafanikio ya kunufaika na fursa hizo yanahitaji wananchi kuwa na uelewa wa masuala ya kifedha, jambo linalofanywa na Benki ya CRDB kupitia programu mbalimbali za elimu ya fedha.

“Kuendelea kuwekeza katika utoaji wa elimu ya fedha kwa wananchi kupitia vipindi vya ubunifu ni dalili tosha kuwa mnatambua na kuwajali wateja wenu,” amesema Makonda.
Amewahimiza Watanzania kutumia kikamilifu elimu hiyo na kuacha kusambaza taarifa zisizo na manufaa kwa jamii.

“Nawasihi sana kuepuka kusambaza taarifa zisizofaa. Badala yake, sambazeni taarifa kuhusu Zogo Mchongo ili elimu hii iwafikie wananchi wengi zaidi,” amesema.
Makonda amesema mpango huo unaunga mkono juhudi za Serikali za kujenga uchumi jumuishi kwa kuongeza uelewa wa kifedha kwa wananchi.

Ameeleza kuwa CRDB imefanikiwa kufikisha elimu hiyo kwa njia mbalimbali zikiwemo televisheni, mitandao ya kijamii, pamoja na kushirikisha wasanii, wanamichezo na watengeneza maudhui, hatua inayorahisisha ujumbe kuwafikia wananchi wengi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Abdulmajid Nsekela, alisema benki hiyo imejipanga kuhakikisha elimu ya fedha inawafikia Watanzania wengi zaidi ili kuwajengea uwezo wa kutumia huduma za kifedha kwa ufanisi.

Amesema kipindi cha CRDB Zogo Mchongo ni sehemu ya mkakati huo, ambapo katika msimu wa nne wananchi watapata elimu kuhusu mikopo, utunzaji na uhifadhi wa fedha, pamoja na matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali.

Dk Nsekela amesema CRDB itaendelea kubuni njia mbalimbali za kufikisha elimu ya fedha kwa wananchi ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi na kuchangia ustawi wa jamii.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button