Ligi Kuu

Dida: Geita Gold itazidi kuwa tishio

DAR ES SALAAM: GEITA Gold imeanza kutuma salamu kwa wapinzani wake baada ya kuonesha ushindani mkubwa dhidi ya Yanga, huku Ofisa Habari wake, Samwel Dida, akisema wanaendelea kujenga kikosi imara kitakachokuwa tishio katika hatua zinazofuata za msimu.

Akizungumza baada ya kichapo cha bao 1-0 kutika kwa Yanga, Dida amesema licha ya kupoteza mchezo huo, kikosi chake kilionesha uwezo mkubwa, hasa baada ya Yanga kubaki na wachezaji 10, ambapo walitawala mpira na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga.

“Kuanzia dakika 65 mpaka mchezo unamalizika, Geita Gold ndiyo ilikuwa ikimiliki mpira. Tumegonga posts zaidi ya tatu na tumepata nafasi nzuri, maana yake tulikuwa tunatengeneza mpango ambao ni mzuri,” amesema Dida.

Amesema hakuna sababu ya kuwalaumu wachezaji kutokana na namna walivyopambana kwa dakika zote 90, akisisitiza kuwa mpango wa kocha ulifanya kazi licha ya timu kushindwa kupata matokeo.

Dida amesema Geita Gold bado haijafikia kiwango ilichokusudia katika ujenzi wa kikosi, lakini mapumziko ya ligi kwa ajili ya michezo ya timu za taifa yatawapa nafasi ya kurekebisha maeneo yanayohitaji maboresho.

“Bado hatujakamilika kwa asilimia 100 kwenye kujenga timu tunayotaka. Mwalimu anaendelea kutengeneza mpango mzuri. Baada ya mechi kadhaa na mapumziko mafupi ya timu ya taifa, kuna vitu vitaongezeka na tutaimarika zaidi,” amesema.

Related Articles

Back to top button