BASATA yawahamasisha wasanii kuandaa kazi za AFCON 2027 kuitangaza Tanzania

DAR ES SALAAM:KAIMU Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bwana Edward Buganga, amewataka wasanii nchini kutumia fursa ya mashindano ya AFCON 2027 kwa kuandaa kazi mbalimbali za sanaa zitakazosaidia kuitangaza Tanzania na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Buganga ametoa wito huo alipokutana na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Foby, katika ofisi za BASATA jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, walijadiliana kuhusu fursa zinazopatikana kupitia sanaa ya muziki kuelekea mashindano ya AFCON 2027 yanayotarajiwa kufanyika nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Buganga alimpongeza Foby kwa kuandaa kazi maalumu kwa ajili ya AFCON 2027 pamoja na kujisajili na kuhuisha kibali chake cha kazi za sanaa. Pia alimhimiza kuendelea kuwa mfano kwa vijana wengine kwa kutumia vipaji vyake katika kukuza tasnia ya muziki nchini.
Aidha, Buganga amewataka wasanii na wadau wote wa sanaa kuhakikisha wanajisajili na kuhuisha vibali vyao ili kutambulika rasmi na kunufaika na fursa mbalimbali zinazotokana na sekta ya sanaa, ambayo imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa na ukuaji wa uchumi.
“Mashindano ya AFCON yanakuja, hivyo wasanii na wadau wa sanaa tujitahidi kuzalisha kazi zitakazoleta tija kwa kuitangaza nchi yetu. Wageni watakapokuja waweze kufurahia Tanzania kupitia kazi za sanaa tunazozalisha huku tukilinda na kuenzi utamaduni wetu,” amesema Buganga.
Kwa upande wake, msanii Foby ameishukuru Serikali kupitia BASATA chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa juhudi zake za kuendeleza sekta ya sanaa nchini na kuwapa vijana fursa zaidi za kujiajiri kupitia vipaji vyao.
“Nimekuwa msanii ninayezingatia taratibu za kazi kwa kujisajili na kuhuisha vibali vyangu.
“Nawahimiza wasanii wenzangu kufanya hivyo, kwani sisi ni kioo cha jamii. AFCON 2027 ni fursa kubwa kwa wasanii kuitangaza Tanzania kupitia kazi zetu na kuonyesha uzalendo wetu,” amesema Foby.
Mashindano ya AFCON 2027 yanatarajiwa kuleta fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii nchini, huku sekta ya sanaa ikitajwa kuwa miongoni mwa maeneo yatakayochangia kwa kiasi kikubwa katika kutangaza utamaduni na vivutio vya Tanzania kimataifa.




