Bodi ya filamu kushirikiana na Arusha artisan Festival

DAR ES SALAAM: BODI ya Filamu Tanzania inatarajia kushiriki katika Tamasha la Arusha Artisan Festival, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa nafasi ya filamu katika kukuza, kuhifadhi na kutangaza sanaa na ubunifu nchini.
Hayo yamebainishwa baada ya Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, kufanya kikao na waandaaji wa tamasha hilo, kujadili ushiriki wa Bodi katika tamasha litakalowakutanisha wadau mbalimbali wa sanaa na ubunifu.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Tanzania International Tourism Festivals, Raju Modha, Mkurugenzi wa Tanzania International Tourism Festivals, Ibrahim Jama, Mratibu wa Arusha Artisan Festival, Andrea Buhuba, pamoja na Kaimu Meneja wa Kitengo cha Uhakiki wa Bodi ya Filamu, Boppe Kyungu.

Katika kikao hicho, wajumbe walijadili namna Bodi ya Filamu itakavyoshiriki katika tamasha hilo na kutumia fursa hiyo kuwaelimisha wadau kuhusu umuhimu wa filamu katika kukuza sekta nyingine za sanaa na ubunifu.
Miongoni mwa shughuli zinazotarajiwa kufanyika wakati wa tamasha hilo ni maonesho ya filamu, yatakayotoa fursa kwa wadau na washiriki kufahamu kazi mbalimbali za filamu.
Pia kutakuwa na mdahalo kuhusu nafasi ya filamu katika kukuza na kuendeleza sanaa nyingine, ikiwa ni pamoja na namna kazi za sanaa zinavyoweza kutumia filamu kama nyenzo ya kufikia hadhira pana zaidi.
Aidha, Bodi inatarajiwa kutoa elimu kwa washiriki kuhusu matumizi ya filamu katika kuhifadhi, kukuza na kutangaza kazi za sanaa, huku ikisisitiza umuhimu wa kutumia ubunifu na teknolojia katika kufikisha kazi hizo kwa jamii.
Ushiriki wa Bodi katika tamasha hilo unatarajiwa kuwa sehemu ya juhudi za kuendelea kuwaunganisha wadau wa filamu na sanaa nyingine, pamoja na kuongeza fursa za elimu na ushirikiano katika sekta ya ubunifu nchini.




