Barker, Ibenge watunishiana misuli

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Simba, Steven Barker, amesema kushindwa kupata matokeo mazuri dhidi ya Azam FC msimu uliopita ilikuwa moja ya sababu kubwa zilizowafanya wakose ubingwa wa Ligi Kuu, akisisitiza awamu hii haitakuwa rahisi wanataka kurekebisha hilo katika mchezo wa kesho.
Simba itakutana na Azam FC kesho Jumatano katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, ikiwa ni mchezo ambao Barker ameupa uzito mkubwa kutokana na malengo ya timu yake msimu huu.
Akizungumza na waandishi wa haabri leo Barker amesema msimu uliopita Simba ilipata pointi moja pekee dhidi ya Azam na mbili dhidi ya Yanga, hali ambayo kwa mtazamo wake ilikuwa na mchango mkubwa katika kuwafanya washindwe kutwaa ubingwa.
Amesema kutokana na hilo, Simba imejiandaa kuhakikisha inapata matokeo mazuri dhidi ya Azam, huku akisisitiza umuhimu wa wachezaji wake kuwa na nguvu, ari na kiwango cha juu cha ushindani katika mchezo huo.
Barker amesema maandalizi ya Simba yamekuwa mazuri licha ya muda mfupi wa mapumziko tangu walipocheza Jumapili, akieleza kuwa wiki iliyopita walifanya maandalizi mazuri kabla ya mchezo wao wa CAF na mafunzo hayo yataendelea kuwasaidia kuelekea Azam.
Hata hivyo, kocha huyo alitambua ubora wa Azam, akisema imeimarisha kikosi chake katika dirisha la usajili na pia ina wachezaji wenye uwezo pamoja na kocha anayejua kazi yake.

Kocha wa Azam FC Florent Ibenge amesema mchezo huo ni miongoni mwa mechi kubwa zaidi Tanzania, akisema kikosi chake kimejiandaa kwa aina hiyo ya ushindani.
Amesema Azam imejiandaa kukabiliana na presha na ushindani wa mechi kubwa, na kwamba timu yake inapenda kucheza michezo yenye ushindani wa kiwango cha juu.




