Rivera: Rwanda haikuwa rahisi

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 Ngorongoro heroes, Mario Rivera, amesema pamoja na Tanzania kupata ushindi wa mabao 3-0, Rwanda ilikuwa timu iliyocheza kwa nguvu na kuendelea kushikilia kiwango chake hadi mwisho wa mchezo
Huo ulikuwa mchezo wa kwanza hatua ya makundi michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ya kuwania nafasi ya AFCON 2027 zitakazofanyika nchini Ghana.
“Haikuwa rahisi kucheza mchezo wa kwanza, hasa ukiwa mwenyeji wa mashindano, lakini wachezaji walicheza kwa kujiamini na walitengeneza nafasi nyingi. Tungeweza kufunga zaidi,” amesema Rivera.
Kocha huyo amesema kingine kilichomfurahisha ni timu yake kutoruhusu bao, akieleza kuwa kutofungwa huko kumeongeza kujiamini kwa safu ya ulinzi kuelekea michezo inayofuata.
Ushindi huo umeipa Tanzania mwanzo mzuri katika harakati za kuwania nafasi ya kushiriki AFCON ya vijana chini ya miaka 20, huku Rivera akisisitiza kuwa kikosi chake kinapaswa kuendelea na kiwango hicho katika michezo inayofuata.




