
MICHUANO ya soka kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika(AFCON) inaendelea leo kwa michezo saba kupigwa viwanja tofauti.
Mabingwa watetezi Senegal itakuwa ugegeni dhidi ya Benin katika kundi L kwenye uwanja wa l’Amitié uliopo jiji la Cotonou, Benin.
Katika kundi K, Afrika Kusini itakuwa mwenyeji wa Morocco mtanange utakaopigwa uwanja wa FNB uliopo jiji la Johannesburg.
Timu ya taifa ya Angola imesafiri hadi jiji la Douala, Cameroon ambako Jamhuri ya Afrika ya Kati itakuwa mwenyeji wa mchezo huo wa kundi E utakaofanyika kwenye uwanja wa La Réunification.
Kivumbi kingine kitakuwa kundi H wakati miamba ya Afrika, Ivory Coast itakuwa mgeni wa Zambia kwenye uwanja wa Levy Mwanawasa uliopo jiji la Ndola.
Katika kundi hilo hilo la H Lesotho itakuwa nyumbani uwanja wa Orlando uliopo jiji la Johannesburg, Afrika Kusini.
Mechi nyingine ya kuvutia itakuwa kundi J kwenye uwanja wa Nuevo uliopo jiji la Malabo wakati wenyeji Equatorial Guinea itakapoikaribisha Tunisia.
Libya itakuwa mgeni wa Botswana katika mchezo mwingine wa kundi J utakaopigwa uwanja wa Obed Itani Chilume uliopo mji wa Francistown.