Mngqithi asifia kiwango cha Mzize

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi amefurahishwa na kurejea kwa mshambuliaji Clement Mzize katika kikosi hicho baada ya kukaa nje kwa takribani miezi saba.
Mzize alipata nafasi ya kucheza mchezo wa jana dhidi ya Geita Gold ikiwa ni mchezo wake wa kwanza msimu huu na kuonesha kiwango kilichomridhisha Mngqithi, ambaye amesema mchezaji huyo bado ni miongoni mwa wachezaji muhimu katika mipango yake.
“Nimefurahi sana kwa sababu naamini ni mmoja wa wachezaji wangu bora. Amefanya vizuri sana kwa mtu aliyekuwa nje kwa miezi saba. Nilifurahi sana na nilitamani angekamilisha kiwango chake kwa kufunga bao,” amesema Mngqithi.
Mngqithi pia ameeleza kuwa anasubiri kurejea kwa Dikson Job ili kuongeza chaguo katika kikosi chake, akisema anahitaji wachezaji hao wote wawe tayari na wenye utimamu wa mwili.
Kocha huyo pia alifafanua kuwa uamuzi wa kuwaacha nje baadhi ya wachezaji muhimu kama Bakari Mwamnyeto na wengine ulikuwa wa makusudi, akisema walihitaji kupumzishwa kutokana na kucheza michezo mingi mfululizo.
Amesema hatua hiyo haikutokana na majeraha, bali ilikuwa sehemu ya mipango ya kuwalinda wachezaji hao dhidi ya uchovu na uwezekano wa kupata majeraha wakati timu ikiendelea na ratiba yake.
Wakati huo huo, kocha huyo amesema kadi nyekundu waliyopata katika mchezo wao wa jana imekuwa sehemu muhimu ya kujenga tabia ya timu hiyo baada ya kuweza kucheza kwa zaidi ya dakika 60 ikiwa na mchezaji mmoja pungufu.
Yanga ililazimika kubadili mipango yake baada ya Aziz Ki kuoneshwa kadi nyekundu na kucheza wakiwa pungufu.
Mngqithi amesema kadi nyekundi imetoa fursa kwa wachezaji wake kupata uzoefu wa kucheza katika mazingira magumu.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC Dar es Salaam Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0.



