AFCONAfrica

NYOTA STARS wanaocheza AFCON kwa mara ya kwanza

TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, inayoshiriki fainali za 34 za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) nchini Ivory Coast inaundwa na wachezaji 27 huku 18 wakishiriki
mashindano hayo kwa mara ya kwanza kabisa.

Huenda hii ikawa ndio timu inayoundwa na wachezaji wengi wageni ambao wanacheza mashindano hayo kwa mara ya kwanza yanayoshirikisha timu 24. Mashindano hayo yanaanza leo Januari 13 hadi Februari 11 nchini Ivory Coast.

Wafuatao ni nyota wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ambao wanaenda kucheza michuano hiyo kwa mara ya kwanza.

Kwesi Kawawa
Kipa huyu mwenye miaka 22 ambaye anacheza soka la kulipwa kwenye kikosi cha
Karlslunds IF, hii ni mara yake ya pili kuitwa kwenye timu ya Taifa ya Tanzania chini ya kocha Adel Amrouche.

Haji Mnoga
Mchezaji wa soka ambaye ana miaka 21 anacheza kama beki wa kulia au winga wa kulia kwa Aldershot Town kwa mkopo kutoka Portsmouth. Alizaliwa England lakini anachezea timu ya taifa ya Tanzania, Mnoga ni zao la akademi ya Portsmouth na ana uzoefu wa kucheza Ligi Kuu ya Daraja la Kwanza, Ligi Kuu ya Daraja la Pili na timu ya taifa
hadi sasa.

Ibrahim Abdulla
Mlinzi tegemeo wa kikosi cha Yanga mwenye umri wa miaka 26 ambaye anacheza kwenye kikosi cha Yanga na mhimili wa safu ya ulinzi ya wananchi. Alianza kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania mwaka 2022, lakini amejihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza chini ya Kocha Adel Amrouche.

Dickson Job
Moja ya wachezaji ambao wamekuzwa na programu za timu za taifa, alikuwa sehemu
ya kikosi cha vijana chini ya miaka 17 kilichocheza fainali za mataifa ya Afrika mwaka
2017.

Morice Abraham
Nahodha wa zamani wa timu ya vijana chini ya miaka 17 aliyeiongoza Tanzania mwaka
2019 na kuonesha kiwango cha hali ya juu na kuzivutia timu nyingi anakipiga kwenye
kikosi cha Spartak Subotica nchini Serbia.

Cyprian Kachwele
Mshambuliaji mwenye miaka 18, anayekipiga kwenye kikosi cha Vancouver Whitecaps cha nchini Canada, ameitwa kujiunga na kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza.

Tarryn Allarakha
Mchezaji wa mpira wa miguu kutoka Tanzania ambaye anachezea timu ya Wealdstone ya Uingereza kama kiungo au winga ambaye ameitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha Taifa Stars.

Beno Kakolanya
Mlinda mlango wa Singida Fountain Gate ambaye amekuwa miongoni mwa makipa
waliojijengea jina kubwa kutokana na kupita kwa miamba ya soka hapa nchini Simba na
Yanga.

Kipa huyu mwenye miaka 29 amekuwa akiitwa mara kadhaa kwenye kikosi cha taifa lakini hii ni mara yake ya kwanza kucheza fainali za mataifa ya Afrika.

Bakari Mwamnyeto
Nahodha wa kikosi cha Yanga ambaye pia ni mhimili kwenye kikosi cha kocha Miguel Gamondi amekuwa na kiwango bora na kukita mizizi kwenye safu ya ulinzi ya wananchi.

Ndio nahodha aliyeweka rekodi ya kuifikisha Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika lakini akiwa amenyanyua makombe sita ya ligi ya ndani.

Lusajo Mwaikenda
Moja ya walinzi bora hivi sasa kwenye Ligi Kuu Bara akiwa na vinara wa Ligi Kuu Bara,
Azam FC, kiraka ambaye anacheza nafasi zote za eneo la ulinzi. Ni miongoni mwa walinzi wanaoenda kucheza fainali za mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza.

Sospeter Bajana
Kiungo wa ulinzi wa Azam ambaye amekuwa mhimili kwenye kikosi cha kocha Youssoupha Dabo, ameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa kwa mara ya kwanza mwaka 2023.
Tayari amefungua akaunti ya mabao akiwa na jezi ya timu ya taifa kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Sudan.

Mzamiru Yassin
Kiungo wa ulinzi wa Simba mwenye rekodi ya kushinda mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi cha Wekundu wa Msimbazi. Nyota huyo mwenye miaka 27 alianza kucheza kwenye kikosi cha Tanzania tangu mwaka 2016 ambapo hadi sasa amecheza michezo 36.

Novatus Miroshi
Alianza safari yake na timu ya taifa ya Tanzania chini ya miaka 20 mnamo Februari 16, 2021, ambapo walipoteza 4-0 dhidi ya Ghana kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika chini ya miaka 20.

Mnamo Septemba 2, 2021, Miroshi aliichezea timu ya taifa ya wakubwa kwa mara ya kwanza katika sare ya 1-1 dhidi ya DR Congo kwenye mchujo wa kufuzu kwa Kombe la Dunia la Fifa 2022. Septemba 7 alifunga bao lake la kwanza dhidi ya Madagascar katika ushindi wa 3-2.

Charles M’mombwa
Mchezaji wa soka wa Kitanzania anayechezea katikati ya uwanja kwa klabu ya Macarthur FC katika ligi ya Australia. Ingawa alizaliwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, anachezea timu ya taifa ya Tanzania.

M’Mombwa aliitwa kujiunga na timu ya taifa ya Tanzania kwa ajili ya mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia la Fifa la mwaka 2026 mwezi Novemba 2023. Alifunga bao pekee la
Tanzania katika mechi yake ya kwanza kabisa, ushindi wa 1-0 dhidi ya Niger mnamo
Novemba 18, 2023.

Kibu Denis
Kiungo mshambuliaji wa Simba ambaye tangu ametua kwenye kikosi hicho amekuwa
kwenye kiwango bora sana. Nyota huyu ambaye alianza kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania mwaka 2021 tayari amecheza michezo 11 huku hii ikiwa ni michuano yake ya kwanza ya mataifa ya Afrika.

Ben Starkie
Mchezaji wa soka wa Kitanzania anayechezea sehemu ya kiungo mshambuliaji katika klabu ya Ilkeston Town kwa mkopo kutoka Alfreton Town. Alizaliwa Leicester, Uingereza. Aliwakilisha Tanzania ya vijana chini ya miaka 20 kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2021.

Pia aliitwa kujiunga na kikosi kikuu cha Tanzania cha wakubwa kwa ajili ya mechi za kirafiki mwezi Machi 2022.

Miano Danilo
Mchezaji wa soka wa Uholanzi anayecheza kama beki wa kulia kwa klabu ya FC Eindhoven ya Uholanzi. Ameitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania chini ya kocha Adel Amrouche.

Mohamed Sagaf
Alizaliwa Somalia, Sagaf alikulia Tanzania mwezi Desemba 2023, aliitwa kujiunga na kikosi cha awali cha timu ya taifa ya Tanzania kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2023.

Mchezaji huyo anachezea klabu ya Boreham Wood katika ligi ya National League
ya Uingereza.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button