“Kuna mtu tunamtafuta”- Fadlu
DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameweka wazi lengo la mechi ya kilele cha Simba day ni kuwa anawapa wachezaji muda wa kucheza uwanjani kuonyesha uwezo wao na muunganiko wa timu yake.
Simba wanatarajia kushuka dimbani kesho dhidi ya APR FC ya Rwanda, katika kilele cha Simba Day, ikiwa ni mara ya kwanza baada ya kutoka Misri walipoweka kambi ya maandalizi ya msimu wa 2024/25 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Fadlu amefurahishwa na uwezo wa wachezaji wake wapya na kupongeza juhudi za timu ya skauti na bodi ya klabu kwa kuunda kikosi mahiri na chenye vipaji wenye utashi wa kupambana.
“Wachezaji wapya waliosajiliwa wana vipaji vya kipekee na wanaleta mtazamo mzuri katika mchezo wetu. Wanaendana kabisa na mtindo wa soka ninaoutarajia kwa Simba. Lengo letu liko wazi, tunalenga kujitoa na kujituma katika kila mashindano, kila mechi ni nafasi ya kupata ushindi na kuirudisha Simba kileleni,” amesema.
Ameongeza kuwa amejiridhisha na kasi ya wachezaji pamoja na kuzoea mbinu zake na wamefanya maandalizi ya timu hiyo kuelekea mchezo wa kesho ambao utampa mwanga wa kuendelea kuboresha timu hiyo kabla ya kuanza msimu.
“Katika muda wa wiki tatu tu, wachezaji wetu wameonyesha uhusiano mkubwa wa kibinafsi na kimbinu uwanjani. Tunapoendelea kufanya kazi pamoja, nina imani tutaona uwiano na ufanisi zaidi. Tumejiandaa kwa kuchambua kwa kina ubora na udhaifu wa wapinzani wetu, na tuko tayari kukabiliana nao na natarajia mechi nzuri,” amesema Kocha Fadlu.