Kocha Dortmund alilia ushindi

DORTMUND: Niko Kovac kocha wa wanafainali wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita Borussia Dortmund atahitaji kukirudisha kikosi chake kwenye njia za ushindi kwenye Bundesliga atakapokuwa nyumbani kuwakabili Union Berlin kesho jumamosi.
Dortmund watakaokikwaa kisiki cha Lille kwenye raundi ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa wamepoteza michezo yao yote ya nyumbani chini ya Kovac aliyechukua mikoba ya kukinoa kikosi hicho mwishoni mwa Januari.
“Tuko nyuma sana, ni lazima tushinde mchezo wa kesho kwa sababu tunahitaji pointi 3 si tu kwa ajili ya kupanda nafazi za juu kwenye msimamo lakini pia ni kwa sisi kama timu na kwa wachezaji kujiamini tena na kuhisi tunaweza kushinda mchezo tena” Kovac amewaambia Wanahabari.
Licha ya kufuzu hatua ya 16 bora UCL, Dortmund hawana muendelezo mzuri kwenye Bundesliga, wameshinda mchezo mmoja pekee katika michezo yao saba iliyopita wakijichimbia katika nafasi ya 11 kwenye msimamo pointi 8 nyuma ya RB Liepzig walio katika nafasi ya 4 ambayo ndio nafasi ya kufuzu kwa ligi ya mabingwa msimu ujao.