Kingwendu, Mafufu warudi CCM

DAR ES SALAAM: WASANII wa muziki na uigizaji wametangaza kurudi Chama cha Mapinduzi CCM huku wakisema kilichowavuta ni hatua kubwa za kimaendeleo zinazotekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Miongoni mwao waliokuwa Chadema yumo Jimmy Mafufu, Rashid Mwishehe ‘Kingwendu’, Shamsa Ford, Aunt Ezekiel, Juma Kassim ‘Juma Nature’, Jacob Steven ‘JB’, Stamina Shorwobenzi na wengine.
Wakizungumza Dar es Salaam leo Mafufu aliyekuwa Chadema amesema amehamia CCM kutokana na mambo mazuri anayofanya Rais Samia akitaja miradi mbalimbali inayogusa makundi yote.
“Tulichokuwa tunapigania ni maendeleo, kwa mara ya kwanza tasnia ya filamu na muziki tumepewa mikopo. Mimi nimepewa mkopo nikiwa mwanachama wa Chadema,
“Zamani hii fani ilikuwa ni fedheha lakini Rais Samia ameiheshimisha, Asante Mama”aliongeza na kusema wanaomtukana ni wajinga.
Amewaita wasanii Ibrahim Mshana ‘Roma Mkatoliki’ na Emanuel Elibariki ‘Ney wa Mitego’ waingie kundini kwani usalama upo kwa wasanii wote.
Akielezea safari yake ya siasa, Kingwendu alisema haikuwa kazi rahisi kwani utajiri wake uliishia kwenye siasa na hakufanikiwa.
Kinngwendu amesema aligombea Ubunge mwaka 2015 na 2020 hakufanikiwa na matokeo yake aliishia kufilisika.
“Nilikuwa na Land Cruiser, Carina, IST na Noah. Naomba pesa ya kampeni eti maji umeshayavulia nguo wewe oga tu,” amesema.
Kingwendu amesema amejiunga CCM tangu mwaka jana baada ya kuona kazi ya Rais Samia inafanyika kikamilifu.
Wasanii hao wanatarajiwa kusafiri nchi nzima kuanzia Machi mwaka huu kwa ajili ya kutangaza mazuri ya Rais Samia.