Jay-Z, Sean Combs wafutiwa kesi ya unyanyasaji wa kijinsia

NEW YORK: MWANAMKE aliyewashutumu wasanii wa Hip-Hop Sean ‘Diddy’ Combs na Shawn Carter maarufu Jay-Z kwa kumnyanyasa kingono alipokuwa na umri wa miaka 13 ametupilia mbali kesi yake ya madai siku ya Ijumaa, rekodi za mahakama zimeonesha.
Jay-Z alishtakiwa mwezi Desemba kwa kumbaka msichana huyo akiwa na Combs kwenye tafrija iliyofuatia Tuzo za Muziki za Video za MTV mnamo Septemba 2000.
Hati iliyowasilishwa kwa Mahakama ya Wilaya ya Marekani kwa Wilaya ya Kusini mwa New York inadai mshtaki ametoa notisi ya kutupilia mbali shitaka hilo kwa hiari, hivyo shauri hilo haliwezi kuwasilishwa tena mahakamani.
Haikuweza kufahamika mara moja iwapo nyota hao walifikia suluhu na mwanamke huyo ambaye hajatambuliwa ama la!
Lakini bilionea mwenye umri wa miaka 55 Jay-Z ameeleza kuwa kesi hiyo ni ya kipuuzi na ya uongo.
“Kesi hii ya madai haikuwa na maana na kamwe haikuenda popote. Hadithi ya kubuniwa waliyotunga ilikuwa ya kuchekesha, wala haikuwa na uzito wa madai hayo,” Jay Z alisema.
“Maumivu ambayo mke wangu, watoto wangu, wapendwa wangu na mimi tumevumilia hayawezi kutupiliwa mbali,”
Malalamiko hayo yameeleza Combs na Carter ambaye ni mume wa supastaa wa muziki wa pop Beyonce walimshambulia mlalamikaji huku mtu mashuhuri mwingine akisimama na kutazama.
“Carter amekuwa na Combs wakati wa matukio mengi yaliyoelezwa humu. Wahusika wote wawili lazima wakabiliane na haki.”
Combs, pia mwenye umri wa miaka 55, ameshtakiwa kando kwa ulanguzi wa ngono na ulaghai. Waendesha mashtaka wa shirikisho wanadai kuwa aliwanyanyasa kingono wanawake na kuwashurutisha kingono, vitendo vilivyochochewa na dawa za kulevya kwa kutumia vitisho na vurugu.
Amekana mashtaka yote, na kesi yake ya jinai kwa sasa imepangwa kuanza Mei 5.