Jahazi la JKT lazidi kuzama Afrika
MWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kufuzu klabu bingwa Ligi ya kikapu Afrika (BAL) JKT amepoteza mchezo wa pili dhidi ya GNBC ya Madagascar kwa pointi 89-72.
Katika mchezo huo dhidi ya GNBC uliochezwa jana usiku kwenye viwanja vya Filbert Bayi Mkuza Kibaha, ulikuwa wenye ushindani mkali baina ya timu zote mbili na kwa mujibu wa Meneja wa timu hiyo Seif Ngowi mchezo ulikuwa wa kwao ila wachezaji walikosa umakini.
“Tuliongoza robo ya kwanza, ya pili walichukua wapinzani lakini ya tatu nan ne tulikimbizana na kutofautiana pointi moja mpaka mbili. Kupoteza kwetu kumetokana na makosa ya wachezaji hawakutaka kufuata maelekezo,”amesema.
Licha ya kupoteza, amesema bado hawajakata tamaa kuna michezo miwili imebaki dhidi ya Nairobi City thunders ya Kenya na Beau Vallo heat ya Ushelisheli wanayotakiwa washinde ili wapate nafasi angalau ya mshindwa bora (best looser) kuvuka hatua ya nane bora.
Anayeongoza kundi ni Urunani BBC ya Burundi aliyeshinda michezo miwili, Nairobi City na GNBC kila mmoja imeshinda mchezo mmoja.
Urunani iliyocheza jana pia, ilishinda kwa pointi 112-43 dhidi ya Beau Vallon heat. Michezo ya leo jioni ni Beau dhidi ya GNBC na Urunani dhidi ya Nairobi City.