Kocha mtoto wa Kurasini heat atamba

DAR ES SALAAM:KOCHA mtoto wa timu ya kikapu Daraja la Kwanza mkoa wa Dar es Salaam Kurasini Heat Godfrey Laswai ‘Brien’ amesema wamejipanga vizuri katika mchezo dhidi ya Polisi kuhakikisha wanashinda.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa kesho kwenye Uwanja wa Bandari Kurasini Dar es Salaam.
Akizungumzia maandalizi ya timu yake kocha huyo mwenye umri wa miaka 12 amesema ana matumaini kikosi chake kitashinda na hivyo, wanapambana kwenye mazoezi kimbinu kujiweka imara.
“Mchezo ujao tumeufanyia mazoezi ya kutosha, timu yetu inafanya maandalizi mazuri kuwakabili Polisi, lengo letu ni kupambana na kushinda mchezo huo,”amesema.
Laswai amesema pamoja na udogo wake wa kufundisha, ameaminiwa na kupewa majukumu na makocha na viongozi wa klabu hiyo.
Amesema mchezo huo alianza kufuatilia akiwa mdogo na baadaye alipelekwa kwenye mafunzo ya ukocha na uamuzi daraja la kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hivyo, habahatishi.
Kurasini heat iko katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 28, ni miongoni mwa timu zinazotarajiwa kutinga hatua ya robo fainali baada ya mzunguko wa 17 na wa mwisho ambao wanahitimisha wikiendi hii.