JKT imeanza vibaya michuano ya Afrika
JKT imeanza vibaya michuano ya kufuzu klabu bingwa Afrika (BAL) kanda ya Mashariki baada ya kukubali kichapo cha jumla ya alama za vikapu 83-60 kutoka kwa Urunani BBC ya Burundi katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye viwanja vya Filbert Bayi mkoani Pwani.
Akizungumza na SpotiLeo Meneja wa timu hiyo Seif Ngowi amesema kilichowaponza hawakuwasoma wapinzani wao mapema kiasi cha kuzidiwa mchezo hasa robo ya kwanza ya mchezo huo.
Kwa mujibu wa Ngowi, robo ya kwanza walifungwa vikapu 29-9 lakini baada ya kusomana, taratibu wakakaa sawa na kushindana na upinzani kwa vikapu 18-17 katika robo ya pili ya mchezo huo.
“Katika robo ya tatu na nne hatukuzidiwa sana lakini kwa sababu tulipotea robo ya kwanza tayari walitudhibiti na kufanikiwa. Lakini bado tuna nafasi ya kurekebisha michezo mingine miwili ili kujihakikishia nafasi ya kufanya vizuri,”amesema.
JKT inatarajiwa kucheza mchezo mwingine leo usiku dhidi ya GNBC ya Madagascar ambapo wameahidi kupambana ili kufanya vizuri.
Ili kufuzu hatua ya nane bora JKT inahitaji kushinda michezo miwili au mitatu katika kundi hilo lenye timu nne.