Mchezaji aiponza Vijana Queens, yafutiwa matokeo
DAR ES SALAAM: TIMU ya Vijana Queens iliyokuwa inashiriki Ligi ya kikapu mkoa wa Dar es salaam imefutiwa matokeo ya mchezo wake namba 504 ilipokuwa inacheza nusu fainali ya pili dhidi ya JKT Stars.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Ufundi na Mashindano ya Chama cha Kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BD), iliyotolewa na Mkurugenzi wa Ufundi na Mashindano Haleluya Kavalambi, sababu ya kufutiwa matokea hayo ni baada ya mchezaji wa Vijana Queens Tupege Lazaro kuonekana amesajiliwa mara mbili na kucheza ligi mbili tofauti ndani ya msimu mmoja ambao ni 2024.
Alisema mchezaji huyo amekiuka kanuni zinazosimamia ligi ya mkoa huo inayozuia mchezaji kusajiliwa na timu mbili tofauti na kucheza ligi mbili ndani ya msimu mmoja.
“Kamati ya Ufundi imekaa na kujiridhisha kwamba mchezaji Tupege Lazaro amesajiliwa timu ya Vijana Queens inayocheza ligi ya mkoa wa Dar es salaam msimu wa 2024 na pia amesajiliwa na timu ya KVZ ya Zanzibar inayocheza ligi ya Unguja msimu wa 2024,”amesema Kavalambi.
Alisema kutokana na kosa hilo mchezaji amekiuka kanuni, kifungu namba 17.3 kinachosema ‘Kutumia mchezaji aliesajiliwa mara mbili ndani ya msimu mmoja’.
“Endapo itagundulika na kuthibitika kuwa timu au klabu imemtumia mchezaji kinyume na kifungu hiki itafutiwa matokeo michezo yote aliyocheza mchezaji huyo.
“Mchezaji huyo atafutiwa usajili na hataruhusiwa kucheza msimu husika na kufungiwa kujihusisha na mpira wa kikapu ndani ya nchi kwa mwaka mmoja,”alifafanua na kuongeza kuwa timu hiyo pia, itatozwa faini ya sh 500,000/=
Kufuatia makosa hayo, timu ya Vijana Queens imefutiwa matokeo dhidi ya JKT Stars hivyo imepokonywa ushindi sasa itacheza mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu dhidi ya DB Troncatti.
Mchezaji Tupege Lazaro amefungiwa kutojihusisha na mpira wa kikapu ndani ya mkoa wa Dar es Salaam kwa muda wa mwaka mmoja na hukumu hiyo imeanza jana, Oktoba 28, 2024.
Kwa mujibu wa Kavalambi, Timu ya JKT Stars itacheza michezo ya fainal dhidi ya Donbosco Lioness. Mchezo wa kwanza utaanza Novemba 05. 2024.