Ilala yang’ara riadha UMITASHUMTA DAR

DAR ES SALAAM: TIMU ya Riadha Kombaini ya Ilala, imeng’ara katika Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA), ngazi ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Mashindano yamefanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, jana na kushirikisha Wilaya tano, Ilala, Temeke, Kinondoni, Ubungo na Kigamboni.
Vijana hao wa Shule za Msingi, walichuana kwenye Mita 100, Mita 100×4 Kupokezana Vijiti ‘Relay’, Mita 200, Mita 400, Mita 800, 1500 na Kiruka Chini ‘Long Jump’.
Timu ya Ilala chini ya Mwalimu Difna Chaila, iling’ara katika matukio mengi huku vijana wakishinda kwa upande wa wasichana na wavulana.
Ilala waliwaburuza wenzao kwenye Mbio za Mita 1500, 800, Mita 100×4 Relay na Kuruka Chini.
Vijana waliochochea ushindi wa Ilala ni pamoja na Samirah Kisava aliyeshinda Mita 800 na 1500, Ikram Namwando na Elizabeth Nyamka Kuruka Chini.
Wilaya iliyofuatia kwa kutoa ushindani kwa Ilala ni Kigamboni huku zikifuatia Temeke, Kinondoni na Ubungo.
Mashindano hayo yaliyosimamiwa na Waamuzi kutoka Chama Cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam (DAA), leo kwa upande wa Mitupo kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Jitegemee.
Mbali na Riadha, Michezo mingine pia iliendelea kwenye viwanja mbalimbali na hitimishwa kwa kupatikana Timu ya Mkoa itayoiwakilisha Dar es Salaam kwenye ngazi ya kitaifa mapema Juni huko mkoani Iringa.



