Michezo MingineRiadha

TAMASHA LA MICHEZO LA KARATU: Ni zaidi ya kuibua vipaji kwa vijana

TAMASHA la 22 la Michezo la Karatu (KSF) limefanyika wiki iliyopita huku likiwa ni zaidi ya
kuibua na kuendeleza vipaji vya wachezaji chipukizi wa michezo mbalimbali.

Tamasha hilo la kila mwaka limekuwa likishirikisha mchezo wa riadha, mpira wa miguu,
mpira wa wavu, ngoma, kwaya na sarakasi na kuchangamsha wakazi wa Karatu na vitongi vyake, ambao wamekuwa wakikusanyika kwenye viwanja vya Mazingira Bora siku ya kilele.

Kwa miaka 22 sasa tamasha hilo limekuwa likifanyika chini ya udhamini wa Olympic Solidarity kupitia Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), lengo likiwa ni kuibua na kuviendeleza vipaji vya michezo mbalimbali na hata kutoa elimu na mafunzo.

KUIBUA VIPAJI
Tamasha la Michezo la Karatu limekuwa likiibua vipaji na hasa vya riadha na kuviendeleza, mfano ni kwa wanariadha kama akina Alphonce Simbu, Gabriel Geay, Failuna Matanga na wengine wengi, ambao wengi wao vipaji vyao vilianza kuonekana katika tamasha hilo.

Wanariadha wamekuwa wakichuana katika umbali tofauti, ambapo wanaume wamekuwa
wakichuana katika mbio za kilometa 10, huku wanawake wenyewe wakitoana jasho katika kilometa tano na watoto wakiume na kike wanachuana katika kilometa 2.5.

Katika mbio za kilometa 2.5 hapa ndiko kwenye uibuaji wa vipaji, hasa kwani wanawashidanisha watoto wa shule za msingi, ambao ndio kiini hasa cha vipaji katika michezo yote.

FILBERT BAYI
Mwanariadha nguli nchini, Filbert Bayi ambaye ni mwenyeji wa Karatu amekuwa akiendesha tamasha hilo kwa lengo la kusaka na kuibua vipaji na kuvifanya kujulikana kwa
wadau wengi wa mchezo wakiwemo makocha.

Bayi amekuwa akitumia taasisi yake ya Filbert Bayi Foundation (FBF), ambayo imekuwa ikifanya kazi ya kila mwaka kupita katika Mashindano ya Shule za Msingi na Sekondari (Umitashumta na Umisseta) na kuchukua wanafunzi waliofanya vizuri katika riadha na
kuwasomesha bure katika shule zake zilizopo Kimara, Dar es Salaam na Mkuza Kibaha mkoani Pwani.

MRATIBU WA TAMASHA
Mratibu wa Tamasha hilo la Karatu, Meta Petro anasema kuwa miaka 22 ya kuendesha tamasha hilo pamoja na changamoto zake, lakini limekuwa na mafanikio mengi hasa kwa
wanariadha chipuizi.

Petro anasema kuwa mbali na wananchi wa Karatu kuburudika kwa kushuhudia michezo
mbalimbali, pia wamekuwa wakipata elimu ya mambo mbalimbali katika jamii kama ufahamu wa ugonjwa wa ukimwi, utunzaji wa mazingira na mengine mengi kupitia katika vikundi vya ngoma, kwaya na hata sarakasi.

Vikundi hivyo vimekuwa vikitumia muda wao kutunga nyimbo za mafunzo au maonyo
mbalimbali kwa jamii, hivyo wakazi wa Karatu na vitongoji vyake, mbali na kupata burudani wamekuwa wakipata elimu kupitia vikundi hivyo.

Anasema vikundi hivyo vimekuwa vikijiandaa sana, kwani kabla ya kupata nafasi ya kutumbuiza katika tamasha hilo, vimekuwa vikichujwa ili vilivyo bora ndio vinapata nafasi hiyo.

Petro anasema kuwa katika mchezo wa soka, timu zimekuwa zikichuana kwa karibu wiki
mbili ambako zimekuwa zikicheza kuanzia katika ngazi ya tarafa na kujichuja hadi kubaki
mbili, ambazo zimekuwa zikicheza fainali, ambayo imekuwa ikifanyika siku moja kabla ya kilele cha tamasha hilo.

WASHINDI MWAKAHUU
Katika mchezo wa riadha kilometa 10 kwa wanaume, mshindi alikuwa John Nahhai wa Geay aliyemaliza mbio hizo kwa muda wa dakika 30:57:64 wakati Mao Nhando alimaliza wa pili kwa dakika 31:09:25 huku mshindi wa tatu ni Boay Dawi aliyetumia dakika 31:23:32.

Katika mbio zakilometa tano wanawake, Magdalena Shauri alitumia dakika 17:32:61 wakati mshindi wa pili ni Hamida Nassoro aliyetumia dakika 17:42:84 na wa tatu ni Jackline Sakilu aliyetumia dakika 18:05:22.

Magdalena na Jackline pamoja na Simbu na Geay tayari wamefuzu kwa Michezo ya Olimpiki
itakayofanyika Paris, Ufaransa mwaka huu kwa upande wa marathoni.

Katika mbio za baiskeli, mshindi alikuwa George Sango wa Shinyanga aliyetumia saa 1:55:28 wakati Amos George alitumia saa 1:55:32 na Noel Solomon wa Arusha alitumia saa 1:55:33.

Katika mbio za watoto za kilometa 2.5, Emmanuel Martin alikuwa wa kwanza kwa wavulana kwa muda wa dakika 8:35:05 huku Isack Josdeph alimaliza wa pili kwa dakika 8:50:51 huku Basaka John akiwa wa tatu kwa dakika 8:58:07.

Kwa wasichana, mshindi wa kwanza alikuwa Kesia Isihaka aliyetumia dakika 9:13:37 huku Noela Loi akiwa wa pili kwa dakika 9:14:93 na Zabrina Hamisi alimaliza wa tatu kwa dakika
9:50:96.

Miaka yote washindi wa michezo ya riadha wamekuwa wakipata zawadi za fedha taslimu huku wale wa michezo ya kitimu kama soka na wavu, wenyewe wamekuwa wakipata
vifaa vya michezo vyenye thamani kubwa.

Related Articles

Back to top button