Majaliwa kuongoza matembezi ya kuokoa Mlima Kilimanjaro

DAR ES SALAAM:WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika matembezi ya kuhamasisha upandaji miti kwa ajili ya kuokoa mazingira ya Mlima Kilimanjaro, yatakayofanyika Mei 17, mwaka huu katika geti la Marangu, mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Nessa, Dobora Nyakisinda, amesema kampeni hiyo inayojulikana kama “Okoa Mlima Kilimanjaro” inalenga kupanda miti bilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la joto duniani, hali inayosababisha kuyeyuka kwa kasi kwa barafu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro.
“Watafiti wanasema katika kipindi cha miaka 30 hadi 50 ijayo, barafu tunayoshuhudia leo huenda ikatoweka kabisa. Ni jukumu letu Watanzania kushirikiana katika kulinda Mlima wetu,” amesema Nyakisinda.
Amesema katika miaka mitano ya awali ya kampeni hiyo, wanatarajia kuanzia na mikoa minne ya Kanda ya Kaskazini ambayo ni Kilimanjaro, Tanga, Manyara na Arusha.
Nyakisinda amefafanua kuwa Mlima Kilimanjaro ni chanzo muhimu cha maji, hewa safi, na kivutio kikuu cha utalii kinachowavutia zaidi ya watalii 65,000 kwa mwaka, hivyo unahitaji kulindwa kwa nguvu zote.
Aidha, ametangaza kuwa kutakuwa na matembezi ya hiari ya umbali wa kilomita 5, 10 na 16 kutoka Marangu hadi Mandara kwa gharama ya ushiriki ya Shilingi 35,000, na kuwataka Watanzania wajitokeze kwa wingi kushiriki.
Kwa upande wake, Ofisa Hifadhi Mwandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Haika Bayona, amepongeza juhudi hizo na kuzitaka taasisi na wananchi kuunga mkono kampeni hiyo.
“Tuunge mkono jitihada hizi. Mtafurahia matembezi haya. Tufuate mfano wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alitembelea Kilimanjaro na kuitangaza nchi yetu kimataifa,” amesema Bayona.
Ameongeza kuwa Mlima Kilimanjaro pia unashiriki katika kampeni ya kutafuta tuzo ya Kivutio Bora Afrika, huku hifadhi za Taifa 10 zikiwa zinawania tuzo nane tofauti.