Vijana 3000 kuchuana Riadha

DAR ES SALAAM: ZAIDI ya wanariadha 3,000 wanatarajiwa kushiriki mashindano makubwa ya vijana yatakayofanyika kesho jijini Dar es Salaam, huku waandaaji wakitarajia kuvutia zaidi ya mashabiki 10,000.
Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam, Amani Ngoka, amewaambia waandishi wa habari Leo kuwa mashindano hayo yatahusisha vijana wenye umri wa chini ya miaka sita hadi 17, yakilenga kutambua, kulea na kukuza vipaji vya riadha mapema.
Ngoka amesema vijana watakaofanya vizuri katika mashindano hayo watapata nafasi ya kuchaguliwa kujiunga na kikosi kitakachoshiriki mashindano ya vijana yatakayofanyika Uganda mwezi ujao.
Ameeleza kuwa baada ya mashindano hayo, vipaji vitakavyobainika vitaendelea kulelewa katika kituo maalum kilichopangwa, ambapo wanariadha hao watanolewa na makocha wazoefu ili kuwajengea uwezo wa ushindani na kuongeza hazina ya vipaji kwa manufaa ya timu ya taifa siku zijazo.
Kwa mujibu wa Ngoka, matarajio yao ni kuona mashindano hayo yakizalisha wanariadha wenye uwezo mkubwa, watakaoweza kufuata nyayo za mastaa wa riadha nchini kama Felix Simbu na wengine walioitangaza Tanzania kimataifa.
“Tunataka kuona vipaji vinaanza kuonekana mapema na kupata mazingira bora ya kuendelezwa ili baadaye viwe nguzo ya taifa katika riadha,” amesema Ngoka.
Amesema mashindano hayo yatakuwa na mbio za mita 100, 200, 400, 800, 1,500 na 5,000, kulingana na makundi ya umri wa washiriki.
Mbali na ushindani wa uwanjani, Ngoka amewashukuru wadau mbalimbali wanaoendelea kuunga mkono juhudi za kukuza riadha ya vijana, akiwemo mfuko wa uwekezaji wa watoto wa UTT AMIS, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) pamoja na Riadha Tanzania.
Kwa upande wake, Ofisa Masoko wa UTT AMIS, Zulfa Hemed, amewahimiza wazazi na walezi kujitokeza kwa wingi kushuhudia na kuwasapoti watoto wao, huku wakitumia fursa hiyo pia kujifunza kuhusu umuhimu wa kuwawekezea watoto wao kwa ajili ya maisha ya baadaye.
Amesema UTT AMIS imeandaa huduma maalum kwa wazazi watakaohitaji kufungua akaunti za uwekezaji kwa watoto, hatua ambayo inaweza kusaidia kuwaandalia msingi mzuri wa elimu na maisha yao ya baadaye.
“Tuna mfuko wa uwekezaji kwa ajili ya mtoto, hivyo mzazi aje ajionee na kushiriki kikamilifu,” amesema Zulfa.



