Gamondi abadili mfumo kuimaliza Azam
DAR ES SALAAM: KOCHA wa Yanga, Miguel Gamondi amesema anaheshimu kila timu na ataingia kwa mfumo wa tofauti katika mchezo wa kesho wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC.
Gamondi amesema Azam wana timu nzuri na kocha mzuri ila watajitahidi kufanya linalowezekana kuhakikisha wanapata alama tatu muhimu.
“Ni matarajio yangu tutacheza mchezo mzuri kuliko michezo iliyopita kila mchezo ni tofauti na mpinzani tofauti itabidi tubadilishe mfumo na tutafute njia na mfumo sahihi kupata matokeo dhidi ya Azam FC, “ amesema Gamondi.
Amesema hakuna muda wa kutosha wa kujiandaa na mchezo lakini wapo tayari kushindana na Azam FC, utakuwa ni mchezo wenye msisimko wa aina yake.
“Kwangu na kwa kocha wa Azam kwani namfahamiana nae kwa miaka 25, utakuwa wasaa mzuri kati yetu, kwenye maisha hupaswi kujiwekea matarajio asilimia mia moja, lolote linaweza kutokea, hiyo ndio tabia ya mpira wa miguu.
Ni kweli tunaweza kukosa wachezaji wengi. Nafahamu Azam wamepata zaidi ya siku saba mpaka nane za kujiandaa. Tumeshacheza michezo miwili wakati wao wakiwa wamepumzika. Lakini nashukuru nimebarikiwa kuwa na wachezaji wazuri sana” amesema Gamondi.