Ligi KuuNyumbani

Simba kumtangaza kocha mkuu kabla ya kwenda Misri

DAR ES SALAAM: TIMU ya Simba ya Msimbazi Jijini Dar es Salaam imeweka wazi kwamba itamtangaza Kocha Mkuu wa kukinoa kikosi hicho na benchi lake la ufundi kabla ya safari yake ya maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu waliyopanga kufanya nchini Misri.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ahmed Ally ameweka wazi kwamba hadi Julai Mosi watakuwa wameshatangaza benchi la ufundi lote na baadhi ya wachezaji wapya watakaoungana na wachezaji wengine kwa ajili ya safari hiyo ya Misri.

Kocha anayezungumzwa sana kupewa nafasi kuiongoza Simba msimu ujao wa 24/25 na kuchukua mikoba ya Abdelhak Benchikha ni raia wa Afrika Kusini Steve Komphela.

Ahmed Ally ameiambia Spotileo kwamba mchakato wa kocha unaendelea vizuri na matarajio yao hadi Julai Mosi, timu inapokwenda nchini Misri itakuwa tayari na kocha pamoja na benchi lake la ufundi.

“Msimu huu tumejipanga vizuri na tunakuja kivingine katika mipango yetu ya kambi hatutaenda kwa mafungu kama ilivyokuwa awali, safari hii tutaenda na kikosi kamili pamoja na benchi la ufundi lililokamilika tukianza kocha mkuu, msaidizi, makipa na watu maalum wanatakiwa kuwepo katika benchi la ufundi,” amesema Ahmed Ally.

Amesema wanasimba wasiwe na presha juu ya ukimya wa klabu yao, kila jambo linaenda vizuri ikiwemo mchakato wa usajili wa wachezaji wapya na mchakato wa kutafuta kocha mkuu mwenye vigezo vilivyowekwa na Simba.

“Tunachukuwa mwalimu atakaye kuja kutuondoa hapa tulipo sasa na kufikia malengo yetu ikiwemo kurejesha heshima ya Simba kwa kutwaa mataji ya ubingwa wa mashindano tunayoshiriki ikiwemo Ligi Kuu Tanzania Bara,” amesema Ahmed.

Related Articles

Back to top button